Na Mwandishi Wetu, Timesmajira
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Balozi Dkt. Pindi Chana amezielekeza Taasisi zilizo chini ya Wizara yake zitoe mafunzo kwa wadau wake ili waweze kuelewa masuala mbalimbali zikiwemo fursa zilizopo katika Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Balozi Pindi Chana ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifanya majumuisho ya Kikao cha Majadiliano Kati ya Wizara na Wadau wa Sekta Binafsi kilichoshirikisha Baraza la Biashara la Taifa (TNBC).
“Vikao na wadau ni muhimu sana katika kujenga uelewa wa pamoja na kusaidiana katika kutatua changamoto, hivyo Serikali chini ya Rais Dkt. Samia imedhamiria kuendeleza Sekta hizi ambazo ni muhimu sana kwa Wananchi,” amesema Balozi Pindi Chana.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. Saidi Yakubu amesema Wizara inaendelea kuboresha muundo wa utekelezaji wa Matamasha mbalimbali ili yaongeze tija na kushirikisha Wasanii wengi.
Ameongeza kuwa, mwaka 2024, Nchi ya Tanzania na China zitakua zinatimiza miaka 60 ya ushirikiano, hivyo zimekubaliana kufanya shughuli 60 za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Shughuli 30 zitafanyika nchini Tanzania na 30 nchini China ambapo wadau wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo watapata fursa ya kushiriki na kuonesha kazi zao.
Katika kikao hicho wadau walipata fursa ya kutoa maoni, ushauri,kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambapo Wataalamu wa Wizara walitoa ufafanuzi na kujibu hoja zilizowasilishwa na wadau hao.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025