October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NEMC yawaonya wanaotapisha vyoo wakati wa masika

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Dar

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na maofisa mazingira wa majiji, manispaa na halmashauri zote hapa nchini wamejipanga kudhibiti wakazi wenye tabia ya kutapisha vyoo hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka, alisema Baraza halitakuwa na huruma wala kurudishwa nyuma na watu wachache ambao wamekuwa kikwazo katika kulinda na kutunza mazingira.

“Hivi karibuni mtakumbuka kuwa nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati na hiyo imetokana na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika nyanja ya uchumi, afya, mazingira na sekta zingine.

Hatutataki kurudi tena zama za kipindupindu hasa katika jiji la Dar es Salaam,” amesema Dkt. Gwamaka.

Katika kuhakikisha wanadhibiti hali ya utapishaji, Dkt. Gwamaka amesema Baraza limejipanga kushirikiana na maofisa mazingira wa majiji, manispaa na halmashauri kudhibiti hali hiyo sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wote.

“Baraza linashirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha maofisa mazingira wa jiji, manispaa na halamashauri zote nchini wanasimamia sheria, taratibu na kanuni za mazingira ikiwemo suala la utapishaji kwenye maeneo ya makazi ya watu,” amesema.

Dkt. Gwamaka amewaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na NEMC hususani kupitia kitengo chake cha timu ya dharura ambacho kinafanya kazi kwa saa 24 kila siku kwani mafanikio makubwa yameshapatikana.

“Wito wangu kwa Watanzania wasichoke kutoa ushirikiano kwa Baraza hasa kwa kitengo chetu cha dharura ambacho kimekuwa kikifanya kazi nzuri kwa saa 24 ili kukabiliana na changamoto za mazingira kwa kuwa watumishi wa chombo hicho hawawezi kuwa kila mahali,’’ amesema.

Aidha, amewashauri Watanzania kuunganisha nguvu ya pamoja kama wanadhani gharama za kutumia magari ya taka ni kubwa ili kuepuka adhabu kali ikiwemo kufikishwa mahamani kwa sababu ya upishaji wa maji taka na utapishaji vyoo.

“Kuna taarifa tunazipata kutoka kwa watu mbalimbali kuwa changamoto inayochangia watu kutapisha vyoo ni gharama za ukodishaji magari ya taka ambayo yamekuwa yakinyonya majitaka katika makazi ya watu.

Nawashauri kuunganisha nguvu ya watu wawili au watatu ili waweze kupata gari ambayo itanyonya majitaka kuliko kuyatiririsha kwenye makazi ya watu kinyume na sheria ya mazingira,” ameeleza.

Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Baraza limendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mazingira yanalindwa ipasavyo ikiwemo kudhibiti uchafuzi wa kelele, kusimamia ipasavyo katazo la mifuko ya plastiki pamoja na udhibiti wa utupaji wa taka hatarishi.