
Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amewaonya wananchi wanaofanya mzaha na kudhihaki tahadhari za Serikali kuhusu mvua za El Niño kupitia mitandao ya kijamii, akisema madhara yaliyotokana na mvua zilizonyesha jijini Mbeya ni ushahidi kuwa suala hilo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
Sagini ametoa onyo hilo Novemba 4, 2026, wakati alipotembelea wananchi walioathiriwa na mafuriko katika Kata ya Nzovwe, jijini Mbeya, ambapo baadhi ya nyumba zimebomolewa na maji huku vyakula na mali nyingine zikisombwa na mafuriko.

Amesema kwa miezi kadhaa Serikali imekuwa ikitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakizipokea kwa mzaha na kejeli kupitia mitandao ya kijamii.
“Niendelee kuwaomba wananchi, miezi kadhaa imepita Serikali imekuwa ikizungumzia mvua za El Niño, lakini watu wengine wamekuwa wakileta mizaha kwenye mitandao ya kijamii, wakisema, ‘mbona wameahidi sana, tunaisubiri El Niño yetu’. Sasa mambo mazito watu wanafanya mizaha. Unaisubiri El Niño sasa iliyotokea Novemba 3, tuiite nini?” amehoji Sagini.
Amesema mvua ya Novemba 3, 2026, ilidumu kwa takribani dakika 30 pekee, lakini ilisababisha madhara makubwa kwa wananchi, akiwataka watu kuomba mvua zinyeshe bila kusababisha majanga badala ya kubeza tahadhari zinazotolewa na wataalamu.
Aidha, amewataka wananchi wa Jiji la Mbeya kuchukua tahadhari na kujiandaa kukabiliana na mvua zinazotarajiwa, akieleza kuwa madhara yaliyotokea baada ya mvua ya nusu saa ni ishara ya hatari inayoweza kujitokeza endapo mvua zitadumu kwa muda mrefu.
“Kwa hiyo, niwaombe upande wa Serikali kuhakikisha watu wanapata miundombinu na sehemu za kuhifadhiwa. Mheshimiwa DC na wakurugenzi wako msibweteke, utaratibu uendelee ili watu wapate mahali pa kukimbilia. Lakini wananchi waliopo kwenye maeneo hatarishi, hizi ni salamu za awali tujiandae, zikija mvua nzito zinazohofiwa na wataalamu wetu tuwe na mahali pa kwenda,” amesema.
Sagini amefafanua kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanapaswa kuanza kuondoka kwa muda katika maeneo hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko, badala ya kusubiri maji yafike kwenye makazi yao.

Amesisitiza kuwa maji yana nguvu kubwa na hivyo wananchi wanapaswa kuweka usalama wao mbele hata katika kipindi ambacho bado wanakabiliana na majonzi yaliyosababishwa na mafuriko.
Kwa upande wake, Josephat Mwanjesa, amemshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na ujumbe wake kwa kuwafikia mapema na kuwafariji waathirika wa mafuriko hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Maafa, mvua hiyo iliyonyesha kwa muda usiozidi dakika 30 imeathiri nyumba 21 na kaya zisizopungua 43.

More Stories
TANESCO yafafanua hitilafu ya Umeme Mbagala, maeneo jirani
e-GA yawataka Maafisa Tehama kuwa na nyaraka muhimu
Dkt.Kijaji atembelea banda la Tanzania maonesho ya WTM