November 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

e-GA yawataka Maafisa Tehama kuwa na nyaraka muhimu

Na Mwandishi wetu

MENEJA wa Usimamizi na Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao (e-GA) Sultana Seiff amewataka Maafisa TEHAMA kuhakikisha taasisi zao zinakuwa na nyaraka muhimu za TEHAMA zinazosaidia kusimamia na kutekeleza ipasavyo Jitihada za Serikali Mtandao

Sultana ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku tano yanayoendelea jijini Dodoma, yanayolenga kutoa uelewa wa pamoja kuhusu Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Usimamizi na Utekelezaji wa Teknolojia Zinazoibukia, ikiwemo Akili Unde (AI), kwa Maafisa TEHAMA.

Meneja huyo amesema kuwa, nyaraka hizo ni pamoja na Sera ya TEHAMA, Mkakati wa TEHAMA, Sera ya Usalama wa TEHAMA, Mpango wa Urejeshaji wa Huduma baada ya Maafa, Sera ya Matumizi Sahihi ya Rasilimali za TEHAMA, Taratibu za Usimamizi wa Huduma za TEHAMA, Taratibu za Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA, Taratibu za Uendelezaji, Ununuzi, Uendeshaji na Matengenezo ya Mifumo ya TEHAMA pamoja na Muundo wa Jumla wa Usanifu wa Mifumo ya Taasisi (Enterprises Architecture).

Amesisitiza kuwa uwepo wa nyaraka hizo ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za TEHAMA zinafanyika kwa kuzingatia taratibu, viwango na miongozo iliyowekwa, sambamba na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa za taasisi za umma.

Aidha, amewahimiza Maafisa TEHAMA kutumia mafunzo hayo kuongeza ujuzi na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia zinazoibukia, hususan Akili Unde, ili kuweza kuzitumia kwa tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Afisa TEHAMA kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Erick Makabali, amesema mafunzo hayo yamemwezesha kupata uelewa wa namna ya kuandaa nyaraka ya Usanifu wa Jumla wa TEHAMA wa Taasisi (Enterprise Architecture), ambayo itasaidia taasisi yake kupanga na kusimamia uwekezaji wa TEHAMA kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa uwepo wa nyaraka hiyo utasaidia MSD kuepuka kujenga au kununua mifumo ya TEHAMA inayotekeleza majukumu yanayofanana, kupunguza gharama zisizo za lazima na kuhakikisha bajeti ya TEHAMA inaelekezwa katika maeneo yenye vipaumbele na mahitaji halisi ya taasisi.

Aidha, amesema mafunzo ya uandaaji wa nyaraka hiyo yatamsaidia kuboresha uratibu na muunganiko wa mifumo ya TEHAMA, kurahisisha usimamizi wa rasilimali za teknolojia na kuimarisha utoaji wa huduma kwa ufanisi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia e-GA za kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika usimamizi na matumizi ya TEHAMA, pamoja na kuendeleza utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini