November 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kivunge ataka madeni yakusanywe kuboresha miundombinu utalii

Na Joyce Kasiki Dodoma


MBUNGE wa Viti Maalum, Marirta Kivunge, ameitaka Serikali kuimarisha ukusanyaji wa madeni yanayodaiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Utalii (TDL), akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuwezesha uwekezaji zaidi katika miundombinu ya utalii nchini.


Akichangia taarifa za Kamati za Bunge kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kivunge amesema kuwa taarifa hiyo imebainisha changamoto katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za TDL, ikiwemo madeni yanayokadiriwa kufikia shilingi milioni 13 ambayo bado hayajakusanywa.


Amesema hali hiyo inahitaji hatua za haraka ili kuhakikisha mapato yote yanayostahili kukusanywa yanaingia serikalini na kutumika kwa maendeleo ya sekta husika.


Kivunge pia ameeleza kutoridhishwa na kiwango kidogo cha fedha kilichotumika kuboresha miundombinu ya utalii, akibainisha kuwa ni asilimia 14 pekee ya fedha zilizotengwa zilizotumika kwa maendeleo hayo, badala ya asilimia 50 iliyokuwa imepangwa.


Amesisitiza kuwa sekta ya utalii ni muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuongeza mapato, hivyo Serikali inapaswa kuhakikisha fedha zinazokusanywa kwa ajili ya maendeleo ya sekta hiyo zinaelekezwa moja kwa moja katika kuboresha miundombinu.


Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu ya The Royal Tour, ambayo imechangia kuongeza mwonekano wa vivutio vya utalii nchini.


Hata hivyo, amesema kuwa kuitangaza Tanzania pekee hakutoshi kuvutia na kuwahudumia watalii ipasavyo bila kuwepo kwa miundombinu bora inayorahisisha upatikanaji wa vivutio na kuboresha huduma wanazopata wageni.
Katika hoja nyingine, Kivunge amezungumzia changamoto ya baadhi ya taasisi za umma kutokuwa na hati za umiliki wa ardhi, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kuathiri usimamizi, ulinzi na matumizi sahihi ya mali za umma.


Amesema ripoti ya CAG imebainisha changamoto hiyo katika taasisi saba zilizokaguliwa, ambazo zina maeneo ambayo hayajakamilishiwa taratibu za usajili na upatikanaji wa hati za umiliki.
Kutokana na hali hiyo, ameitaka Serikali kuhakikisha taasisi hizo zinakamilisha taratibu za usajili na kupata hati za umiliki wa ardhi ili kulinda mali za umma na kuhakikisha ardhi inatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.