Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Chunya
WANANCHI wa Kijiji cha Mpembe, Kata ya Lualaje, wilayani Chunya mkoani Mbeya, wamejikuta wakilazimika kujenga vivuko vyao wenyewe ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, kufuatia ukosefu wa vivuko vya uhakika katika eneo hilo.
Hata hivyo, vivuko hivyo vinavyomilikiwa na baadhi ya wananchi vinatoza fedha kwa kila mtu anayevuka, hali inayoongeza mzigo wa gharama kwa wananchi, hususan wagonjwa na watu wenye kipato cha chini.
Akizungumzia changamoto hiyo, Diwani wa Kata ya Lualaje katika Jimbo la Lupa, Leckson Mwakasuluka, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imejipanga kujenga vivuko vyote vinne vilivyopo katika eneo hilo ndani ya kipindi cha miaka mitano ili kuwaondolea wananchi adha hiyo.

Mwakasuluka amesema changamoto hiyo inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi, kutokana na umuhimu wa Kijiji cha Mpembe kiuchumi, kikitegemea zaidi shughuli za kilimo, ufugaji na biashara.
Amesema zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya Halmashauri yanatokana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika eneo hilo, hivyo ni muhimu kuwepo kwa miundombinu bora ya vivuko ili kurahisisha shughuli za uzalishaji na biashara.
Amesema kutokana na kukosekana kwa vivuko vya uhakika, baadhi ya wananchi wameamua kujenga vivuko vyao na kutoza fedha kwa watumiaji, jambo linalowalazimu wananchi kulipia kila wanapohitaji kuvuka.
“Wananchi wanaotembea kwa miguu wanalipa Sh2,000, huku wanaotumia bodaboda wakitozwa Sh5,000. Hii imekuwa adha kubwa, kwani hata mtu anapokuwa mgonjwa, kwa mfano ana malaria na anahitaji kuvuka kwenda upande mwingine, bado analazimika kulipa fedha hizo. Hali hii inaumiza wananchi,” amesema Mwakasuluka.

Aidha, amesema kwa kushirikiana na Halmashauri wamejipanga kutatua changamoto hiyo kwa kujenga vivuko vyote vinne ndani ya miaka mitano, huku hatua za awali zikilenga kuanza na kivuko kimoja ili wananchi waanze kupata huduma kwa urahisi.
Ameeleza kuwa tayari wameomba Sh16 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko hivyo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utasaidia kupunguza gharama za kuvuka na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa Mpembe.


More Stories
Waziri Mkuu wa Rwanda avutiwa na bidhaa za Tanzania
Tanzania yatumia ISA kuvutia Uwekezaji wa Nishati ya Jua
PATA MATOKEO YA DARASA LA SABA HAPA