
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imetoa wito kwa vijana na wadau wengine kujikita katika shughuli mbalimbali za kilimo ili kujiongezea kipato na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Mamlaka hiyo imesema kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi na chanzo muhimu cha ajira, huku kikitoa malighafi kwa viwanda na fursa za kibiashara zinazoweza kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza na Timesmajira Online Oktoba 23, 2026, katika maonesho ya biashara na uwekezaji ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Gombe jijini Mbeya, Afisa Kilimo Mwandamizi wa COPRA, Joshua Musimu, amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

Amesema maonesho hayo ni fursa kwa wakulima, wafanyabiashara, wanafunzi na wadau wengine kujifunza kuhusu uzalishaji, usimamizi na biashara ya mazao mbalimbali ya kilimo.
“Ili kutimiza Dira ya 2050, wadau wote, wakiwemo vijana, wanapaswa kujihusisha na shughuli za kilimo kwa sababu sekta hiyo ina manufaa makubwa, inatoa ajira na kuzalisha malighafi mbalimbali zinazohitajika katika shughuli za kiuchumi,” amesema Musimu.
Amesema mwanzoni mwa maonesho hayo idadi ya watu waliotembelea banda la COPRA ilikuwa ndogo, lakini mwamko umeendelea kuongezeka kadiri siku zinavyosonga, huku wananchi, wafanyabiashara, vyuo na wanafunzi wakifika kupata elimu kuhusu shughuli za mamlaka hiyo.

Hata hivyo, amesema mwitikio wa wakulima bado hauridhishi, hali ambayo huenda ikatokana na uhamasishaji mdogo. Ameongeza kuwa usambazaji wa vipeperushi umeanza kuongeza uelewa na kuvutia wadau zaidi kutembelea banda hilo.
Kwa mujibu wa Musimu, wafanyabiashara wengi wanaotembelea banda la COPRA wanahitaji ufafanuzi kuhusu taratibu za kufanya biashara ya mazao, ikiwemo usajili na upatikanaji wa vibali vya kusafirisha mazao.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo Mkuu Daraja la Pili wa COPRA, Benedicta Chuwa amesema mamlaka hiyo inasimamia minada ya kidijitali ya mazao mbalimbali, yakiwemo kakao, soya, ufuta, choroko na ndengu.
Amesema katika maeneo ambayo bado hayajaanzisha minada ya kidijitali, hususan maeneo ya mipakani kama Tunduma na Kasumulu, mamlaka imeweka utaratibu wa kufuatilia biashara ya mazao ili kuhakikisha inatambulika na kufanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Ameeleza kuwa wafanyabiashara wanaonunua mazao na kufuata taratibu za COPRA hupatiwa vibali vinavyowawezesha kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi.
Naye Lucy Abraham, mkazi wa Ilomba jijini Mbeya, ambaye ametembelea maonesho hayo, amesema ni muhimu kwa wananchi kupata fursa za kujifunza kuhusu biashara na uwekezaji, lakini changamoto ya usafiri imeathiri mahudhurio ya baadhi ya watu.
Amesema mgomo wa madereva wa bajaji umekuwa kikwazo kwa baadhi ya wananchi na wakulima waliotaka kutembelea maonesho hayo ili kujifunza kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi.


More Stories
Mfumo kidijiti kuondoa urasimu bima afya kwa wote
PPAA yaelimisha wabunifu, wakadiriaji kuhusu zabuni za umma
Wanafunzi Babati watakiwa kuwa mabalozi wa Utalii / Uhifadhi