October 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo kidijiti kuondoa urasimu bima afya kwa wote

Na Moses Ng’wat, Tunduma.

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu, amesema matumizi ya mfumo wa kidijitali katika Bima ya Afya kwa Wote yanatarajiwa kuondoa urasimu wa makaratasi, kuharakisha taarifa za matibabu na kurahisisha malipo kwa vituo vya kutolea huduma za afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Bima ya Afya kwa Wote, uliofanyika Oktoba 22, 2026, katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Dkt. Kasululu alisema mfumo huo utawezesha taarifa za matibabu kuwasilishwa moja kwa moja kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Alisema mfumo huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma kwa kuwezesha vituo vya afya kupata fedha kwa wakati, hali itakayosaidia ununuzi wa dawa na mahitaji mengine muhimu ya matibabu.

Kuhusu gharama, Dkt. Kasululu alisema kaya yenye watu wasiozidi sita inaweza kuchangia Shilingi 150,000 kwa mwaka ili kupata huduma za afya kwa kipindi hicho.

Kwa kaya yenye watu sita, gharama hiyo ni wastani wa Shilingi 25,000 kwa kila mtu kwa mwaka.

Alisisitiza kuwa watoa huduma za afya mkoani Songwe wako tayari kutekeleza mpango huo kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki kwa wakati.