September 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Azania Benki kuinua wananchi kwa riba ndogo

Na Joyce Kasiki, Geita

WAJASIRIAMALI mkoani Geita wamepata fursa ya kukopa hadi Shilingi milioni 500 kwa riba ya asilimia moja kwa kipindi cha miaka mitano kupitia Azania Bank, huku mkopaji akirejesha Shilingi milioni 2.75 kwa mwezi.

Akizungumza Septemba 28, 2026 kwenye Siku ya Mabenki katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Meya wa Manispaa ya Geita, Leonard Bugomole, amesema mkopo huo unalenga kuwawezesha wajasiriamali kukuza mitaji yao na kushiriki katika biashara ya kimataifa.

Bugomole amesema fursa hiyo imefunguliwa chini ya sera ya Serikali ya kuwezesha sekta binafsi kupata mitaji nafuu, na amewataka wafanyabiashara kuitumia ipasavyo kuagiza bidhaa na kuanzisha viwanda vidogo.

Amesema Azania Bank pia imeanzisha huduma ya CIP Lounge (Commercially Important Person) kwa wateja wa kibiashara, inayolenga kutoa huduma ya haraka na ya heshima kwa wajasiriamali.

Kwa upande wake, Meneja wa Azania Bank Tawi la Geita, Rhoda Baluhya, amesema benki hiyo inaendelea kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali wadogo, ikiwemo mkopo wa Shilingi laki moja kwa riba ya Shilingi 6,000 kwa mwaka.

Baluhya amesema kaulimbiu ya benki hiyo ya “Benki inayozidisha matarajio yako” inalenga kuwapa wateja huduma zinazokidhi mahitaji ya biashara zao.

Naye mfanyabiashara Peresencia Chanzi wa kampuni ya Lausnicho Company LTD amesema amewahi kunufaika na huduma za Azania Bank, ikiwemo kupata elimu ya biashara, kuunganishwa na wenye viwanda nchini China na kupata mikopo ya kununua mashine za kiwandani.

Chanzi amesema benki hiyo imekuwa ikimhudumia kwa haraka pale anapohitaji kufanya malipo ya mizigo bandarini, na amewashauri wanawake na vijana kuchangamkia fursa za mikopo na huduma za kuweka akiba, ikiwemo akaunti za watoto.