Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
KAMPUNI ya Uendelezaji wa Gridi ya Taifa (ETDCO) imewahimiza wadau na kampuni zinazojihusisha na uchimbaji wa madini kutumia fursa zinazotolewa na kampuni hiyo katika ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya umeme kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
Akizungumza jana Mkoani Geita katika maonesho ya Madini, Kaimu Meneja wa Mipango na Uhakiki wa Ubora wa ETDCO,Kaimu Meneja wa Mipango na Uhakiki wa Ubora wa ETDCO,Mha.Masule Masanga amesema wadau wanaojihusisha na miundombinu ya umeme, hususan usambazaji na usafirishaji wa umeme mdogo na mkubwa, wanaendelea kutafuta fursa za kushirikiana na kampuni za uchimbaji madini katika kuhakikisha zinapata huduma ya umeme inayokidhi mahitaji yao.

Amesema Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa maeneo yenye shughuli nyingi za uchimbaji wa madini, hivyo kuna fursa kubwa kwa kampuni za uchimbaji kushirikiana na ETDCO katika ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Kwa upande wake, mdau wa sekta ya madini, Muhunda Nyakiloto, amesema kampuni za uchimbaji madini ambazo bado hazijaweka miundombinu ya umeme zinapaswa kuchukua hatua mapema, kwani kuchelewa kunaweza kuongeza muda na gharama za utekelezaji wa miradi.

Ameshauri kampuni hizo kuwasiliana na ETDCO kwa ajili ya kupata utafiti, ushauri wa kitaalamu na mipango sahihi ya namna ya kuweka miundombinu ya umeme kulingana na mahitaji ya shughuli zao za uzalishaji.
Naye Sadamu Samali, Electrical Supervisor wa GGM, ameishukuru ETDCO kwa kutembelea kampuni hiyo na kushirikiana katika uendelezaji wa miundombinu ya umeme.
“Tunashukuru ETDCO kwa kututembelea na kuvuta laini ya umeme. Kama kampuni tunathamini ushirikiano huu,”amesema Samali.

Hatua hiyo ilielezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya umeme na sekta ya madini, ili kuhakikisha mahitaji ya nishati yanaendana na kasi ya shughuli za uzalishaji katika Kanda ya Ziwa.

More Stories
Wakina mama wahimizwa kufanya mazoezi
TIRA yang’ara, yatunukiwa tuzo ya pili
Sheikh Jongo akemea chuki za udini