July 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaweka mazingira rafiki kuvutia uwekezaji sekta ya elimu

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka mikakati ya kuimarisha ushiriki wa sekta zingine katika uwekezaji wa elimu, ikisema hatua hiyo ni muhimu kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Imesema hatua hiyo inalenga kuongeza rasilimali za maendeleo ya sekta ya elimu huku serikali ikiendelea kuboresha sera, kanuni na mifumo ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji kushiriki katika utoaji wa huduma za elimu nchini.

Akizungumza jijini hapa leo Julai 13,2026 katika kikao  cha mwaka cha Menejimenti ya Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 cha tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha uliopita na maandalizi ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/27,Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof.Carolyne Nombo alisema  sekta ya elimu ina nafasi ya msingi katika kufanikisha Dira 2050 kwa kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesema Dira 2050 inaelekeza kuwa asilimia 30 ya uwekezaji itatokana na serikali, huku asilimia 70 ikitarajiwa kutoka sekta binafsi, jambo linaloifanya Wizara  kuweka mazingira yatakayorahisisha ushiriki wa wawekezaji katika sekta hiyo.

Aidha ametaja lengo la mkutano huo kuwa ni kupokea na kujadili wasilisho la kitaalam kuhusu nafasi ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika utekelezaji wa Dira 2050,kupokea na kujadili wasilisho kuhusu mbinu mbadala za ufadhili na ugharamiaji wa Elimu ua Juu.

Kupokea na kujadili wasilisho kuhusu umuhimu na tija ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuendesha shughuli za serikali .

Prof.Nombo amebainisha kuwa Taasisi  za udhibiti zinaendelea kupitia na kuboresha kanuni mbalimbali ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kukwamisha uwekezaji binafsi, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Aidha,amesema serikali imebaini fursa nyingi za uwekezaji katika Vyuo Vikuu na kampasi 16 zilizopo maeneo mbalimbali nchini ambazo, licha ya kuwa na miundombinu ya kufundishia, bado zinahitaji nyumba za watumishi na mabweni ya wanafunzi.

“Maeneo hayo yanatoa nafasi kwa sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu muhimu ambayo itaongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia,”amesema.

Pia Prof.Nombo amesema  Wizara inaendelea kutafakari mbinu mbadala za upatikanaji wa fedha kupitia mapendekezo yaliyowasilishwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa bajeti ya serikali na kuongeza vyanzo vya fedha kwa ajili ya maendeleo ya elimu.

Pamoja na hayo amesisitiza Taasisi za Elimu kuanzisha na kuimarisha shughuli za kuzalisha mapato kupitia miradi mbalimbali ya kiuchumi pamoja na ushirikiano na sekta binafsi ili kuongeza uwezo wa kujitegemea kifedha.

Vilevile,Wizara imeeleza  kuwa itaendelea kusimamia utekelezaji wa mpango wa ushirikiano kati ya waajiri na Vyuo  vya kati,Vyuo vya ufundi stadi na Vyuo vikuu, ukiwa na lengo la kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo Prof.Nombo amesisistiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ni utekelezaji wenye mafanikio wa Dira 2050 na kuifanya elimu kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya Tanzania.