Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono wawekezaji wanaowekeza katika sekta ya usafiri, hususan wanaoleta teknolojia ya usafiri wa umeme, akisema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuboresha sekta ya usafiri, kulinda mazingira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa pikipiki na bajaji za umeme kutoka Kampuni ya Plug & Ride Company Ltd, Kihenzile amesema Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wenye teknolojia bunifu zinazochochea maendeleo ya Taifa.
“Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili teknolojia za kisasa kama hizi ziweze kukua nchini. Matumizi ya usafiri wa umeme yatasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kupunguza utegemezi wa mafuta, kulinda mazingira na wakati huo huo kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema Kihenzile.
Amesema uwekezaji huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji kutoka sekta binafsi na kuharakisha matumizi ya nishati safi katika sekta ya usafiri.
“Tunataka kuona Tanzania inakuwa kitovu cha teknolojia za kisasa za usafiri barani Afrika. Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wanaokuja na ubunifu unaowanufaisha wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla,” ameongeza Kihenzile.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, amesema ushirikiano kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje ni ushahidi wa mafanikio ya sera za Serikali zinazolenga kukuza uwekezaji na kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Dkt. Msemwa amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha miradi yenye tija inaendelea kuanzishwa nchini na kutoa manufaa kwa wananchi.
“Uwekezaji tunaouona leo ni matokeo ya sera nzuri za Serikali zinazoweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi. Ushirikiano huu unaonyesha kuwa Tanzania ni sehemu salama na yenye fursa nyingi kwa wawekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi,” amesema Dkt. Msemwa.
Aidha, amewataka vijana kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa kujifunza teknolojia mpya, kuanzisha biashara na kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

“Ninawahimiza vijana kuchangamkia fursa zinazotokana na uwekezaji huu. Teknolojia mpya zinahitaji nguvu kazi yenye ubunifu na ujuzi, hivyo ni wakati wa vijana kujitokeza na kushiriki katika kujenga uchumi wa Taifa,” ameongeza.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Plug & Ride Company Ltd, Otieno Igogo, amesema kampuni hiyo imejipanga kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri nchini kwa kuhamasisha matumizi ya pikipiki na bajaji za umeme ambazo ni nafuu zaidi kuendesha kuliko zinazotumia mafuta ya petroli na dizeli.
Amesema matumizi ya teknolojia ya umeme yatasaidia kupunguza gharama za usafiri kwa waendesha bodaboda na bajaji, huku yakichangia kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya mafuta.

“Dhamira yetu ni kubadilisha mfumo wa usafiri nchini kwa kuleta teknolojia rafiki kwa mazingira na yenye gharama nafuu kwa wananchi. Tunaamini usafiri wa umeme ndiyo mustakabali wa sekta hii, na Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na mabadiliko hayo,” amesema Igogo.
Ameeleza kuwa bidhaa zilizozinduliwa ni pamoja na pikipiki na bajaji za umeme zinazoweza kutumika kwa usafirishaji wa abiria, mizigo, wagonjwa na wanafunzi, huku zikiwa zimetengenezwa kwa teknolojia kutoka India na kuunganishwa nchini na Watanzania.
“Teknolojia tunayoiingiza nchini inatoka India, lakini hatua ya kuunganisha vifaa inafanyika hapa Tanzania. Hii inaongeza ajira, inakuza ujuzi wa Watanzania na inaweka msingi wa maendeleo ya sekta ya utengenezaji wa vifaa vya usafiri wa umeme nchini,” amesema Igogo.
Amesisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia usafiri wa umeme wenye gharama nafuu, salama na rafiki kwa mazingira.

More Stories
Serikali yaweka mazingira rafiki kuvutia uwekezaji sekta ya elimu
Mixx yakabidhi zawadi kwa washindi watatu Sabasaba
Wananchi watakiwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi