
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline ,Mbeya
WANANCHI wamehimizwa kuendelea kutunza mazingira kwa kutumia bidhaa zinazotengenezwa kwa malighafi za asili, ikiwemo mikeka ya kusokotwa kwa mkono, ambayo huchangia kupunguza matumizi ya bidhaa zisizo rafiki kwa mazingira huku ikitoa fursa za kuongeza kipato kwa wananchi.
Wito huo umetolewa Julai 10, 2026 na Spika Mstaafu wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dk. Tulia Ackson, baada ya kumtembelea ,Enelesta Pili, mkazi wa Mtaa wa Isengo, Kata ya Iyela, jijini Mbeya, ambaye amekuwa akijishughulisha na usukaji wa mikeka kwa miaka mingi na kutumia kipaji hicho kujipatia kipato na kuendesha maisha yake.

Dk. Tulia amempongeza Enelesta kwa ubunifu wake, akisema kazi za mikono zinazozalisha bidhaa za asili zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa familia na wakati huo huo kulinda mazingira.
Ameeleza kuwa matumizi ya mikeka ya plastiki yamekuwa yakiongezeka katika maeneo mengi, lakini bidhaa hizo zinapoharibika huwa haziozi kirahisi na hivyo kuchangia uchafuzi wa mazingira.
Amesema mikeka inayosukwa kwa kutumia malighafi za asili huoza baada ya kutumika na hatimaye kuwa sehemu ya mbolea, jambo linalochangia uhifadhi wa mazingira.
“Bibi yetu, pamoja na kusuka mikeka hii, anatufundisha namna ya kutunza mazingira naomba wananchi waige mfano huu kwa kujifunza kusuka na kutumia mikeka ya asili. Bidhaa hizi ni rafiki kwa mazingira na zinasaidia kuhifadhi mazingira yetu kwa vizazi vijavyo,” alksema Dk. Tulia.
Kwa upande wake, Enelesta amesema usukaji wa mikeka si chanzo cha kipato pekee, bali pia ni njia ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa za asili ambazo ni salama kwa mazingira na zinapaswa kuthaminiwa na Watanzania.
Naye mjukuu wake, Getruda Kassim, amesema aliamua kuchapisha video ya kazi ya bibi yake kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuitangaza ili iwafikie wateja wengi zaidi, sanjari na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za asili zinazozalishwa nchini.

“Nilichapisha video hiyo ili nimsaidie bibi yangu kupata soko la kazi zake, lakini pia kuwahamasisha Watanzania kuthamini bidhaa zetu za asili ambazo zinachangia utunzaji wa mazingira,” amesema Getruda.
Kutokana na umaarufu uliotokana na video hiyo, Enelesta amepokea zawadi ya Sh milioni moja baada ya kubuni na kusuka mkeka wenye jina la Dk. Tulia Ackson, kazi iliyovutia watu wengi kupitia mitandao ya kijamii na kuwa mfano wa jinsi vipaji vya jadi vinavyoweza kufungua fursa za kiuchumi na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.

More Stories
Diamond: Usimamizi wa sheria waongeza uwekezaji sekta ya habari
JAB yazindua mwongozo wa Ithibati ya maisha kwa Waandishi Wakongwe
BRELA yaibua fursa mpya ulinzi wa Alama za Biashara