
Na Moses Ng’wat, Mbozi.
SERIKALI imewaonya wafanyabiashara wanaouza pembejeo zisizokidhi viwango (feki) na wanaojihusisha na utoroshaji wa mbolea ya ruzuku kwenda nchi jirani, ikisema vitendo hivyo ni hujuma kwa taifa na kwamba wanaovifanya hawana tofauti na wauaji kutokana na athari zake kwa uzalishaji wa chakula, usalama wa chakula na uchumi wa nchi.
Akizungumza na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo na mifugo wa Mkoa wa Songwe Julai 10, 2026, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wote watakaobainika kuuza pembejeo feki, kutorosha au kuficha mbolea ya ruzuku, pamoja na kupandisha bei kiholela.

Alisema wafanyabiashara watakaokiuka sheria watafutiwa leseni na kuchukuliwa hatua za kisheria, akisisitiza kuwa fedha zinazowekezwa na Serikali kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea lazima ziwafikie walengwa na kuleta tija katika sekta ya kilimo.
Chongolo aliwataka wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa uadilifu kwa kuuza mbolea kwa bei elekezi, kutunza kumbukumbu sahihi na kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia biashara ya pembejeo. Pia amewahakikishia ushirikiano wafanyabiashara waaminifu.
Alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Agenda 10/30, huku mpango wa ruzuku ya mbolea ukilenga kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza malighafi za viwandani na kuinua kipato cha wakulima.

Aidha, aliwahakikishia wakulima kuwa hakuna upungufu wa mbolea nchini, akieleza kuwa kwa sasa zipo tani 248,617 za mbolea za aina mbalimbali, huku tani nyingine 313,800 zikitarajiwa kuingia nchini kati ya Julai na Septemba mwaka huu.
Pia alisema TFRA imelenga kuhakikisha tani milioni 1.5 za mbolea zinapatikana katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili kukidhi mahitaji ya wakulima wote.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Mbozi, Onesmo Mkondya, aliibua hoja ya changamoto ya upatikanaji wa mbolea ya ruzuku, akisema hadi sasa ni kampuni moja tu inayodaiwa kuingiza mbolea hiyo mkoani Songwe, hali iliyozua hofu kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, alisema tatizo la wauzaji wa pembejeo na mbegu feki limeendelea kuwa sugu na kuitaka Serikali kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya wahusika.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Pembejeo, Boniface Masika, alimuomba Waziri kuzuia makampuni ya mbolea kuuza bidhaa hizo moja kwa moja kwa wakulima na, badala yake, vitumie mfumo wa mawakala.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, alimhakikishia Waziri kuwa mkoa umejipanga kikamilifu kudhibiti hujuma zote zinazohusu pembejeo za kilimo.

More Stories
Diamond: Usimamizi wa sheria waongeza uwekezaji sekta ya habari
JAB yazindua mwongozo wa Ithibati ya maisha kwa Waandishi Wakongwe
Wananchi wahimizwa matumizi bidhaa za asili kulinda mazingira