July 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tutuba apongeaza kiatamizi IAA ,ataka mfano uigwe


Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kuanzisha Kiatamizi cha Biashara (IAA Business Start Up Centre) kinachowawezesha wanafunzi kubuni na kuendeleza mawazo ya biashara, hatua inayowasaidia kujiajiri, kuajiri wengine na kujikwamua kiuchumi mara wanapohitimu masomo yao bila kutegemea ajira za Serikali.


Tutuba alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la IAA katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo alipata maelezo kuhusu namna kiatamizi hicho kinavyofanya kazi na mafanikio yake katika kuwaandaa wanafunzi kuwa wajasiriamali.


Alisema juhudi zinazofanywa na IAA ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za elimu ya juu kwani zinawawezesha vijana kutumia elimu yao kujenga biashara zenye tija na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.


“Nawapongeza kwa namna mnavyokiendesha kiatamizi hiki,ninaamini wengi wataendelea kuja kujifunza hapa, na hata wale waliopitia katika programu hii wanaendelea kutoa ushuhuda mzuri wa mafanikio walikofikia hukonwaliko,” alisema Tutuba.


Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano na Masoko wa IAA, Sarah Goroi, alisema mbali na kuwa na mitaala inayokidhi mahitaji ya soko la ajira, taasisi hiyo imejikita pia katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara kupitia kiatamizi hicho IAA Business Start Up Centre.


“Mbali na kuwapa elimu ya darasani, tunawasaidia wanafunzi kuanzisha miradi yao ya biashara,wapo ambao tayari wameanzisha biashara ndogondogo zinazokua vizuri, na pale tunapobaini mwanafunzi ana kipaji au wazo zuri la biashara, tunaanza kulikuza hadi linakuwa biashara halisi,” alisema Goroi.


Aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha mwanafunzi anapohitimu anakuwa tayari ana biashara au bidhaa inayoweza kuingiza kipato, hivyo kumwezesha kujitegemea na kuwa mwajiri badala ya kusubiri ajira.


Goroi alisema tangu kuanzishwa kiatamizi hicho , zaidi ya vijana 8,600 wamenufaika , ambapo kati yao wanafunzi 1,520 waliibua mawazo mbalimbali ya biashara na kufanikiwa kuanzisha biashara zaidi ya 50.


Alisema kati ya biashara hizo, kampuni 11 zilisajiliwa rasmi na zinaendelea kufanya shughuli zake katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, ubunifu wa teknolojia, sanaa,uhifadhi , uhifadhi wa mazingira na maeneo mengine ya uzalishaji.


Kwa mujibu wa Goroi, kampuni hizo zimeendelea kutoa fursa za ajira kwa wahitimu na vijana wengine, huku zikichangia kukuza uchumi na kuhamasisha utamaduni wa ujasiriamali nchini.


Alibainisha kuwa IAA imeendelea kusimamia na kuwakuza wanafunzi kupitia kiatamizi hicho tangu kilipozinduliwa mwaka 2020, na kwamba mafanikio yaliyopatikana yanaonyesha umuhimu wa kuunganisha elimu na ubunifu katika kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea.