Na Joyce Kasiki
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho amesema ulinzi wa amani unaotekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) unaendelea kuweka mazingira salama yanayowezesha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo na uzalishaji mali.
Akizungumza Julai 6, 2026, alipotembelea banda la JKT katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Nyansaho alisema pamoja na jukumu la kulinda taifa, JKT kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali (SUMAJKT) linaendelea kutoa mchango mkubwa katika kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.
Alisema kampuni tanzu za SUMAJKT zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuwapatia vijana fursa za ajira huku zikichangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali.
Akitoa mfano, alisema Kampuni ya Usafi na Unyunyizi Dawa ya SUMAJKT (SUMAJKT Cleaning and Fumigation Company Limited) imefanikiwa kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 4,000 Watanzania.
“JKT kupitia SUMAJKT limeendelea kuonyesha namna taasisi za umma zinavyoweza kushiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na utoaji wa ajira kwa vijana, jambo ambalo ni muhimu katika kupunguza ombwe la ajira nchini,” alisema Dkt. Nyansaho.
Aidha, aliwapongeza JWTZ na JKT kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kulinda taifa na kudumisha amani, huku akiwahamasisha wananchi kutembelea banda la JKT katika maonesho ya Sabasaba kujifunza kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na jeshi hilo kupitia vikosi, makambi, shule, chuo na kampuni tanzu za SUMAJKT.

More Stories
Dkt. Lekashingo ataka utafiti wa kina Sekta ya Madini
Ndejembi ajadili awamu ya pili ya mradi wa umeme wa jua kishapu
Airtel yaweka alama ruaha Marathon 2026