July 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa utalii waaswa kujiandaa kunufaika na Afcon 2027

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imesema inaendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kama jukwaa la kuhamasisha utalii wa ndani, kutangaza vivutio vya utalii na kuwaandaa wadau wa sekta hiyo kunufaika na fursa zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Utalii Mwandamizi wa TTB, Naomi Mbilinyi, amesema maonesho ya Sabasaba yamekuwa fursa muhimu kwa taasisi hiyo kuwafikia wananchi na kuwapa elimu kuhusu huduma na fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii.

Amesema kupitia banda la TTB, wananchi wanapata taarifa kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini pamoja na fursa za uwekezaji na uendeshaji wa biashara za utalii, ikiwemo kuanzisha kampuni za utalii na kushiriki maonesho ya kimataifa.

Mbilinyi amesema TTB pia inatumia maonesho hayo kutangaza Swahili International Tourism Expo (S!TE) inayotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, huku wadau wakipewa fursa ya kujisajili kama waoneshaji, washiriki na wadhamini wa maonesho hayo.

Aidha, alisema bodi hiyo inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia kwa kuandaa mfumo wa kidijitali utakaowezesha wadau wa sekta ya utalii kusajili taarifa za biashara zao na kutangaza huduma zao kwa urahisi katika masoko ya ndani na kimataifa.

Kuhusu maandalizi ya AFCON, Mbilinyi amesema TTB imeweka eneo maalum katika banda lake kwa ajili ya kutoa elimu kwa watoa huduma mbalimbali kuhusu namna ya kujiandaa kupokea wageni wengi watakaotembelea Tanzania wakati wa mashindano hayo.

Amesema huduma za malazi, usafiri, migahawa na shughuli nyingine zinazohusiana na utalii zinatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na mashindano hayo, hivyo wadau wanapaswa kujiandaa mapema kutumia fursa hizo.

Mbilinyi amesema kuwa wananchi wengi wanaotembelea banda la TTB wamekuwa wakionesha hamasa ya kutaka kufahamu zaidi maeneo ya utalii yaliyopo karibu na makazi yao, hususan fukwe, makumbusho, maeneo ya kihistoria na vivutio vinavyofaa kwa safari za siku moja.

Amesema wananchi pia wamekuwa wakitaka kupata taarifa kuhusu gharama za kutembelea hifadhi za taifa na vivutio vingine, ambapo TTB kwa kushirikiana na taasisi za sekta ya utalii huwapatia maelezo sahihi na kuwaelekeza kwa watoa huduma husika.

Ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la TTB katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu fursa za utalii, mifumo ya kidijitali inayotayarishwa na bodi hiyo pamoja na maandalizi ya AFCON na maonesho ya kimataifa ya utalii.

Amesisitiza kuwa maonesho hayo yanatoa nafasi kwa wananchi kuzungumza moja kwa moja na wataalamu wa sekta ya utalii, kupata mwongozo na kufahamu fursa mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta hiyo nchini.