June 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Matumizi magari ya umeme kuongeza umuhimu gesi asilia

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),Mhandisi Charles Sangweni amesema mwenendo wa matumizi ya nishati duniani unaonesha kuwa katika miaka ijayo matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli yanaweza kupungua kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuongezeka kwa matumizi ya magari ya umeme pamoja na yale yanayotumia gesi asilia.

Mha. Sangweni ameyasema hayo jijini hapa leo Juni 23, 2026 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, akibainisha kuwa mabadiliko hayo ya matumizi ya nishati yanaifanya gesi asilia kuwa rasilimali muhimu katika kipindi hiki cha mpito wa nishati duniani.

Amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kunufaika na mabadiliko hayo kutokana na kuwa na akiba kubwa ya gesi asilia inayoweza kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mha. Sangweni, ongezeko la matumizi ya gesi asilia linaweza kuchangia ukuaji wa uchumi, kuongeza uwekezaji katika sekta ya nishati na kuimarisha upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya gesi asilia ili kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali hiyo huku ikichangia jitihada za kulinda mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.

Pamoja na hayo Mha.Sangweni ameeleza kuwa PURA inafanya kazi chini ya Wizara ya Nishati na ina  majukumu matatu,ambapo amefafanua jukumu la kwanza ni kuishauri Serikali kuhusu shughuli zote zinazohusu mkondo wa juu wa Petroli,jukumu la pili ni kumshauri Waziri mwenye dhamana ya nishati kwani ilikuwa chini ya Wizara ya Nishati  na Madini lakini jukumu lingine ni kusimamia shughuli zote zinazotekelezwa kwenye mkondo wa juu wa Petroli.

“ Petroli ni mjumuisho wa mafuta na gesi,gesi asilia LPG,mafuta au mgao wa Petroli huwa yanachimbwa chini kama ilivyo madini,unapochimba huwezi kujua kama unapata ni kipi unaweza kupata mafuta,gesi au maji,”amesema