June 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yataka ulinzi,uwezeshaji wajane

Na Oscar Tarimo WMJWM Dodoma

SERIKALI imezitaka familia, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wajane wanalindwa, wanaheshimiwa na kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na Taifa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janet Mayanja kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yanayoadhimishwa Juni 23, 2026 chini ya kaulimbiu isemayo “Imarisha Haki, Utu na Uwezeshaji Kiuchumi kwa Wajane.”

Akisoma hotuba ya Waziri Dkt. Gwajima, Mayanja amesema wajane ni kundi muhimu katika jamii kutokana na mchango wao katika malezi ya familia, uzalishaji mali na maendeleo ya Taifa, huku akibainisha kuwa bado baadhi yao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kunyimwa haki za urithi, kunyang’anywa mali, kutengwa na jamii na kukosa fursa za kiuchumi.

Aidha amesema Serikali inaendelea kuhimiza ulinzi wa haki za wajane kwa kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza makazi, ardhi au mali kutokana na kifo cha mwenza wake, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuachana na mila, desturi na imani potofu zinazochangia unyanyapaa dhidi ya wajane.

Pia, amewahamasisha wajane kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali, vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri na fursa za zabuni za asilimia 30 za ununuzi wa umma zinazotengwa kwa makundi maalum ili kuimarisha hali zao za kiuchumi.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdunoor, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza afua zinazolenga kuboresha maisha ya wajane, ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu haki za urithi, uwezeshaji wa kiuchumi na uimarishaji wa mifumo ya ulinzi na ustawi wa jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yanalenga kuhamasisha jamii kutambua mchango wa wajane katika maendeleo na kuongeza juhudi za kuwalinda dhidi ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, huku Serikali ikisisitiza dhamira yake ya kujenga jamii yenye usawa, haki, utu na maendeleo endelevu kwa wote.