June 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCB yazindua Kampeni ya ‘Tuma Bure, Shinda Kila Wiki’

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Benki ya DCB imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini, ambapo imezindua kampeni maalum ya miezi sita ijulikanayo kama “Tuma Bure, Shinda Kila Wiki” inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali na kuwapatia wateja nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali huku wakifanya miamala bila kutozwa gharama.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Sabasaba Moshingi, amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika matumizi ya huduma rasmi za kifedha sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia mifumo ya kisasa ya kifedha.

“Lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini kwa kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za benki kwa urahisi, usalama na gharama nafuu kupitia mifumo ya kidijitali,” amesema Moshingi.

Amesema Benki ya DCB imefanya maboresho makubwa ya huduma zake za kidijitali baada ya kubaini kuwa wateja wengi wanahitaji huduma za haraka, salama, nafuu na zinazopatikana muda wote.

“Sekta ya fedha inaendelea kubadilika kwa kasi kubwa duniani kote. Wateja wetu wanahitaji huduma ambazo ni rahisi, za haraka, salama na zinazopatikana muda wote. Kutokana na mabadiliko hayo, Benki ya DCB ilifanya tafiti mbalimbali kuona namna bora ya kuendeleza huduma zitakazokidhi matarajio ya wateja wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa tafiti hizo zilionesha kuwa wateja wanahitaji huduma zenye gharama nafuu, hali iliyosababisha benki hiyo kufanya mageuzi makubwa katika huduma zake za kidijitali.

“Katika tafiti hizo tuligundua kuwa wateja wetu wanahitaji huduma nafuu zaidi. Kwa sababu hiyo, Benki ya DCB imefanya mageuzi makubwa ya huduma zake za kidijitali kwa kuweka mifumo ya kisasa inayowezesha huduma kupatikana kwa urahisi kwa wananchi wengi zaidi,” amesema.

Moshingi amesema kupitia mfumo mpya wa DCB Pesa App, wateja wanaweza kufungua akaunti popote walipo nchini na kufanya miamala mbalimbali bila makato.

“DCB imejikita katika safari ya mageuzi ya kidijitali ili kuhakikisha wateja wanaweza kujifungulia akaunti popote walipo. Kwa sasa tuna wateja nchi nzima, na dhamira yetu ni kuhakikisha huduma zetu zinaendelea kuwafikia Watanzania wote,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko wa DCB, Geofrey Magugi, amesema mteja anayefungua akaunti kupitia DCB Pesa App na kufanya angalau muamala mmoja ataingia kwenye droo ya kila wiki yenye zawadi ya Shilingi 100,000 kwa washindi 10.

“Mteja anayefungua akaunti kupitia DCB Pesa App na kufanya angalau muamala mmoja ataingia kwenye droo ya kila wiki ambapo washindi 10 watapata Shilingi 100,000 kila mmoja. Aidha, wateja watakaofanya miamala zaidi ya mitatu kwa mwezi watapata nafasi ya kushinda zawadi kubwa zaidi ikiwemo Shilingi milioni moja kila mwezi,” amesema Magugi.

Naye Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Ramadhani Mganga, amesema kampeni hiyo itadumu hadi Desemba mwaka huu na inalenga kuwazawadia wateja wanaotumia huduma za benki kwa njia za kidijitali.

“Kampeni hii itadumu hadi mwezi Desemba mwaka huu na inalenga kuwazawadia wateja wanaotumia huduma za benki kwa njia za kidijitali. DCB imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi za fedha zinazoweka kipaumbele katika ubunifu wa huduma nafuu huku ikitoa fursa kwa Watanzania kufungua akaunti na kufanya miamala kutoka mahali popote nchini bila kulazimika kutembelea matawi ya benki,” amesema Mganga.

Ameongeza kuwa pamoja na faida ya kutuma fedha bila makato, washiriki wa kampeni hiyo watapata nafasi ya kushinda zawadi za kila wiki, kila mwezi pamoja na zawadi kubwa itakayotolewa mwishoni mwa kampeni mwezi Desemba.

“Tunawaalika Watanzania kuchangamkia fursa hii kwa kufungua akaunti za DCB na kutumia huduma zake za kidijitali ili kufurahia huduma za kifedha kwa urahisi zaidi pamoja na nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali,” amesema.