Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
MIFUKO ya uwekezaji inayosimamiwa na iTrust Finance Limited imeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa, huku thamani ya mali zinazowekezwa ikiongezeka kutoka Shilingi bilioni 50 wakati wa kuanzishwa kwake mwezi Desemba 2024 hadi kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 550 kwa sasa.
Ukuaji huo unaashiria kuongezeka kwa mwitikio wa Watanzania katika uwekezaji wa pamoja (Unit Trust Funds), ambao unaendelea kuwa njia mbadala ya kujenga utajiri na ustawi wa kifedha wa muda mrefu.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wawekezaji wa mifuko ya iTrust uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa iTrust Finance, Prof. Mohamed Warsame, amesema mifuko hiyo imeendelea kutoa matokeo chanya kupitia uwekezaji katika hisa, hati fungani na vyombo vingine vya kifedha vinavyopatikana katika soko la mitaji.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na kuimarika kwa usimamizi wa uwekezaji pamoja na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wanaoendelea kujiunga na mifuko hiyo.

Prof. Warsame amebainisha kuwa pamoja na ukuaji huo, bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja na kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji.
Aidha,amesema iTrust imefanikiwa kuendeleza mfumo wake wa kidijitali kwa kutumia wataalamu wa Kitanzania pekee, hatua inayodhihirisha uwezo wa wataalamu wa ndani katika kubuni na kutekeleza suluhisho za kisasa za huduma za kifedha.

Mkutano huo uliwakutanisha wawekezaji waliohudhuria ana kwa ana pamoja na wengine walioshiriki kwa njia ya mtandao, ambapo walipata fursa ya kujadili utendaji wa mifuko yao na mustakabali wa uwekezaji wao.
Kwa upande wake, Mhasibu wa Mfuko wa iTrust, Francis Samkyi, amesema mkutano huo ulihusisha mifuko mitano ya uwekezaji inayosimamiwa na kampuni hiyo ambayo ni iCash Fund, iSave Fund, iIncome Fund, iGrowth Fund na Iman Fund.
Ameeleza kuwa wawekezaji walijadili utendaji wa mifuko hiyo na kupitisha maboresho mbalimbali yaliyolenga kuongeza ufanisi wa uwekezaji pamoja na kuongeza thamani kwa wanachama wa mifuko hiyo.
Samkyi amesema iGrowth Fund huwekeza katika hisa na hati fungani zenye kiwango cha kati cha hatari, wakati Iman Fund huendeshwa kwa kuzingatia misingi ya Sharia za Kiislamu ili kukidhi mahitaji ya wawekezaji wanaopendelea mfumo huo.

Ameongeza kuwa iTrust inaendelea kuboresha huduma zake na kupanua fursa za uwekezaji kwa lengo la kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuchangia maendeleo ya sekta ya masoko ya mitaji nchini.

More Stories
Mikoa minne kupata Umeme wa Gridi 2026/27
Serikali yapongezwa uwekezaji mkubwa wa Kituo cha Kufua Umeme JNHPP
Airtel  yaimarisha mawasiliano vijiji Vitatu