Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Yas Fiber Tanzania itawekeza takribani shilingi bilioni 300 katika kipindi cha miaka 20 kwa ajili ya kupanua huduma za intaneti yenye kasi visiwani Zanzibar kufuatia kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar na Yas Fiber.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Miundombinu ya kidijitali ni msingi wa uchumi wa kisasa. Ushirikiano huu utaharakisha mageuzi ya kidijitali na kusaidia kuiweka Zanzibar katika nafasi ya kuwa miongoni mwa vinara wa uchumi wa kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Soraga.

Amesema mradi huo utasaidia kupunguza pengo la kidijitali kwa kuwaunganisha wananchi wengi zaidi kwenye huduma za mawasiliano na kufungua fursa za elimu, biashara, ubunifu na ajira kwa vijana.
Uwekezaji huo unatarajiwa kuwezesha huduma za mkonga wa mawasiliano (Fiber-to-the-Home – FTTH) kuwafikia takribani kaya 100,000 katika visiwa vya Unguja na Pemba ndani ya miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji wake.

Makubaliano hayo yanaashiria hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha miundombinu ya kidijitali Zanzibar na kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti za uhakika, nafuu na zenye kasi kwa kaya, biashara, taasisi za elimu, vituo vya afya na taasisi za serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, amesema ushirikiano huo utaongeza kasi ya upanuzi wa huduma ya mkonga wa mawasiliano visiwani humo na kusaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi.
“Ushirikiano huu utawezesha wananchi na taasisi nyingi zaidi kupata huduma za intaneti yenye kasi na kuchangia ujenzi wa miundombinu ya kidijitali inayohitajika kwa maendeleo ya Zanzibar ya sasa na ya baadaye,” amesema Mhandisi Suleiman.

Ameongeza kuwa huduma ya mkonga majumbani itatoa mbadala wa uhakika, wa kasi na wenye gharama nafuu zaidi kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea huduma za intaneti kupitia mitandao ya simu.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Fiber, Maxime Woimant, amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya kampuni hiyo katika kuunga mkono ajenda ya mageuzi ya kidijitali na maendeleo jumuishi kupitia mawasiliano ya kisasa.

“Huu ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa miundombinu ya kidijitali kuwahi kufanyika Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni. Kupitia ushirikiano huu, tutapanua upatikanaji wa huduma za intaneti za viwango vya kimataifa zitakazowezesha biashara kukua, wanafunzi kujifunza na jamii kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” amesema Woimant.
Amesema katika miaka mitatu ya kwanza Yas Fiber inalenga kuunganisha takribani kaya 100,000 na huduma za intaneti ya kasi huku biashara, taasisi na wananchi wakinufaika na huduma bora na nafuu zaidi.
“Yas Fiber inajiona si mwekezaji pekee bali mshirika wa maendeleo wa muda mrefu anayelenga kupanua fursa za kijamii na kiuchumi kupitia mawasiliano ya uhakika na ya kisasa,” ameongeza.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Hawa Mbaye, akisoma hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa malengo ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano bora, rahisi na za gharama nafuu.
“Makubaliano haya yanakuja katika wakati mwafaka ambapo serikali inaendelea kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kidijitali na kujenga uchumi unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia. Tunatarajia kuona ongezeko la maeneo yanayofikiwa na huduma za mkonga pamoja na kuimarika kwa ubora wa huduma za intaneti majumbani,” amesema.
Mradi huo utatekelezwa chini ya mfumo wa Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ukiunganisha maono ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga uchumi wa kidijitali na uzoefu wa Yas Fiber katika kubuni, kuwekeza, kujenga, kuendesha na kusimamia huduma za Fiber-to-the-Home (FTTH).
Mbali na uwekezaji wa miundombinu, ushirikiano huo pia utachangia maendeleo ya ujuzi wa kidijitali, uhamishaji wa maarifa na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, hatua itakayosaidia kuandaa kizazi kijacho kushindana katika uchumi unaoendeshwa na teknolojia na kuunga mkono maono ya muda mrefu ya Zanzibar ya kuwa kitovu cha uchumi wa kidijitali Afrika Mashariki.

More Stories
Mikoa minne kupata Umeme wa Gridi 2026/27
Serikali yapongezwa uwekezaji mkubwa wa Kituo cha Kufua Umeme JNHPP
Airtel yaimarisha mawasiliano vijiji Vitatu