June 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPAA yataja mafanikio mfumo mpya kuahughulikia malalamiko

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAMLAKA ya Rufani za Zabuni za Umma (PPAA) imesema matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa malalamiko ya zabuni yameleta mabadiliko makubwa kwa wazabuni na taasisi za umma, huku yakirahisisha utoaji wa haki na kuongeza uwazi katika mchakato wa rufani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea  eneo la Chinangali jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, ameaema mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia malalamiko ya zabuni ambao ulianza kutumika mapema mwaka 2025 umeongeza kasi ya utatuzi wa mashauri na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu.

Sando ameeeza kuwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, mamlaka hiyo imeendelea kupokea na kufanyia kazi malalamiko mbalimbali yanayotumwa kwa njia ya mfumo huo kutoka taasisi za serikali pamoja na wazabuni waliosajiliwa.

Kwa mujibu wake, mfumo huo umeunganishwa na mfumo wa NeST, jambo linalowezesha wadau wote wa zabuni kushiriki na kufuatilia hatua za mashauri yao kwa urahisi zaidi bila ulazima wa kufika katika ofisi za mamlaka husika.

Amefafanua kuwa hapo awali wazabuni walikabiliwa na changamoto za kutumia muda mrefu na gharama za usafiri kufuatilia mwenendo wa malalamiko yao, lakini sasa huduma nyingi zinapatikana kwa njia ya mtandao.

Aidha, ameema mfumo huo umeimarisha utunzaji wa nyaraka za zabuni kwa kuhifadhi taarifa zote muhimu katika sehemu moja, hatua inayorahisisha upatikanaji wa vielelezo vinavyohitajika wakati wa kusikiliza na kuamua mashauri.