June 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yahamasisha matumizi nishati safi

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

MKURUGENZI  Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yamekuwa fursa muhimu kwa shirika hilo kuwaelimisha wananchi kuhusu shughuli zake, ikiwemo mchakato mzima wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme hadi kumfikia mtumiaji wa mwisho.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la TANESCOna mbanda mengine ya masuala ya nishati  katika maonesho hayo yanayofanyika jijini Dodoma katika viwanja vya Chinangali , Twange anesema shirika limeonyesha mifano mbalimbali ya miundombinu ya umeme ili kuwapa wananchi uelewa mpana kuhusu huduma zinazotolewa na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Amesema moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika maonesho hayo ni utekelezaji wa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo TANESCO imejiwekea lengo la kufikia asilimia 20 ya matumizi ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2034, kutoka kiwango cha takribani asilimia tano kilichopo sasa.

Kwa mujibu wa Twange, shirika linaendelea kuhamasisha matumizi ya majiko ya umeme kwa kuweka utaratibu wa kuyakopesha wananchi kupitia mfumo wa kulipa kidogo kidogo wanaponunua umeme, huku likitarajia kusambaza takribani majiko milioni moja katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo kwa ushirikiano na wadau wa sekta binafsi.

Aidha, ameaema TANESCO inaunga mkono matumizi ya umeme katika sekta ya usafiri kwa kuhamasisha matumizi ya baiskeli, pikipiki, bajaji na magari yanayotumia umeme, sambamba na kufunga vituo vya kuchajia magari hayo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwaondolea hofu watumiaji na wawekezaji.

Twange amesema Tanzania, kama kitovu cha usafiri na biashara kwa nchi kadhaa jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam, imejipanga kuhakikisha miundombinu ya kuchajia magari ya umeme inapatikana katika korido mbalimbali za usafirishaji ili kurahisisha matumizi ya teknolojia hiyo.

Akizungumzia mafanikio ya shirika, amesema TANESCO kwa sasa ina wateja wanaokaribia milioni 6.2 na uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 4,000 za umeme, huku mafanikio hayo yakichangiwa na juhudi za watumishi zaidi ya 12,000 wanaofanya kazi katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.

Katika hatua nyingine, Twange amesema TANESCO inaendelea kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo kuzindua mfumo wa mawasiliano unaotumia akili mnemba (AI Chatbot) mwezi Julai mwaka huu, utakaowezesha wateja kupata majibu ya maswali yao kwa haraka zaidi pamoja na kuendelea kutumia namba ya huduma kwa wateja 180 kwa mawasiliano na ufafanuzi wa huduma mbalimbali.