Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, amesema Serikali ina mpango wa kuhakikisha kuwa katika Jimbo la Lupembe kunajengwa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, ikiwemo zao la parachichi, ili kuongeza thamani ya mazao hayo na kuwanufaisha wakulima.
Akijibu swali la Mbunge wa Lupembe, Edwin Swale,leo Mei 26,Bungeni jijini Dodoma aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga viwanda vya parachichi katika jimbo hilo, Londo amesema tayari Serikali imetenga eneo lenye jumla ya ekari 79,293.62 kwa ajili ya kilimo na ujenzi wa viwanda.
Amefafanua kuwa eneo hilo liko katika Kijiji cha Ikang’asi, Kata ya Mfriga, Tarafa ya Lupembe mkoani Njombe, ambapo Serikali inalenga kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo hususan parachichi.
“Ndani ya miaka mitano, Serikali inalenga kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda yanawekewa miundombinu ya msingi ili kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda hivyo,” amesema Londo.
Katika swali la nyongeza, Mbunge Swale amesema Jimbo la Lupembe pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Njombe ni maeneo yanayolima kwa kiwango kikubwa zao la parachichi na yana maeneo mengi ya uwekezaji, lakini sehemu kubwa ya matunda hayo huharibika kutokana na kukosekana kwa viwanda vya usindikaji.
Alihoji iwapo Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha kongani za viwanda ili kuwanusuru wakulima dhidi ya upotevu wa mazao yao.
Akijibu swali hilo, Londo amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaona umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika viwanda vya parachichi, huku akibainisha kuwa ndani ya Mkoa wa Njombe tayari kuna viwanda vya kuongeza thamani ya zao hilo.
Aidha, anewataka wananchi na wakulima kutumia fursa zinazotolewa kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima pamoja na Benki ya Kilimo ili kupata mitaji ya kuwekeza katika kilimo na kuongeza thamani ya zao la parachichi kupitia usindikaji.

More Stories
Mwaselela ahamasisha ujenzi uzio Iyela
Wanahabari wahimizwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi
REA yaandika historia Ludewa