May 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA  yatoa utabiri wake  msimu wa Juni hadi Agosti 2026

Na Mwandishi wetu,Timesmajira 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa wa msimu wa Kipupwe wa Juni hadi Agosti (JJA) mwaka 2026.

Msimu huo unatarajiwa kutawaliwa na hali ya baridi katika maeneo mengi ya nchi, huku mwezi Julai ukitajwa kuwa na vipindi vya baridi kali zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza utabiri huo, leo Mei 25, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema maeneo mbalimbali ya Tanzania yatashuhudia viwango tofauti vya hali ya joto, upepo pamoja na vipindi vya mvua nje ya msimu.

Dkt. Chang’a amesema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini, Nyanda za Juu Kusini-Magharibi pamoja na Mkoa wa Singida.

Aidha, amesema maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini na maeneo ya nchi kavu, Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki, Ukanda wa Pwani ya Kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani.

Dkt. Chang’a amesema kuna baadhi ya maeneo yatapata vipindi vya mvua nje ya msimu, hususan maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria, hasa Mkoa wa Mara, maeneo ya mwambao wa pwani na maeneo ya nchi kavu, visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo yenye miinuko katika Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki.

“Msimu wa Kipupwe wa mwaka 2026 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa Kusini Mashariki uliopungua nguvu kidogo kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi ya nchi huku vipindi vya upepo mkali kutoka kusini vinatarajiwa kujitokeza zaidi katika miezi ya Juni na Julai, hasa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu. Amesema.