Na Mwandishi Wetu, Timesmajjira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, imezindua rasmi kampeni yake mpya ya ‘Zingatia Mtandao wa Viwango’, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kuimarisha mtandao na kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za kidijitali.
Kupitia kampeni hiyo, Yas inalenga kuwahamasisha Watanzania kutambua thamani halisi ya kutumia mtandao unaozingatia viwango vya ubora – mtandao unaowezesha mawasiliano bora, intaneti ya kasi, na huduma za kidijitali kwa uhakika.
Uzinduzi huu unaenda sambamba na mafanikio makubwa ya Yas katika uwekezaji wa miundombinu, ambapo kampuni imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 1 katika upanuzi na uboreshaji wa mtandao wake, na hivyo kuufanya kuwa miongoni mwa mtandao ulioenea zaidi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa Yas Tanzania, Emmanuel Mallya, amesema
baada ya kujenga mtandao imara, sasa wanataka Watanzania wanufaike zaidi – iwe ni kwenye shughuli za kiuchumi, elimu, burudani, kilimo au mawasiliano ya kila siku
Amesema, Yas ina zaidi ya minara 4,800 – takribani minara 1,000 zaidi ya mtoa huduma anayefuatia, hatua inayowezesha kufikia zaidi ya asilimia 95 ya Watanzania mijini na vijijini.
Mbali na upanuzi wa minara, Yas pia imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya fiber na kuimarisha teknolojia ya mtandao wake kutoka 2G hadi 4G, pamoja na kuanzisha huduma za 5G katika miji ya kimkakati.
Maboresho hayo yanaongeza kasi, ubora na uthabiti wa mawasiliano kwa wateja.
Ubora wa mtandao wa Yas umethibitishwa kimataifa na kampuni ya Ookla, inayojulikana kwa upimaji wa kasi ya intaneti kupitia Speedtest.
Yas imetambuliwa kuwa mtandao wenye kasi zaidi nchini kwa miaka mitatu mfululizo.
“Mtandao wa Viwango siyo kasi tu – ni uwezo wa Watanzania kufanya zaidi kila siku, popote walipo. Leo, mteja wa Yas anaweza kufanya biashara mtandaoni kwa ufanisi, kujifunza bila vikwazo, na kufurahia burudani bila kusuasua,” amesisitiza Mallya.
Kupitia kampeni hiyo, Yas inaweka msingi mpya wa matumizi ya mtandao nchini, ambapo mtandao hauishii kuwa huduma pekee, bali unakuwa nyenzo muhimu ya kufungua fursa za kiuchumi, elimu na maendeleo kwa kila Mtanzania.

More Stories
Nkasi yapokea boti ya chanjo kuimarisha huduma mwambao, ziwa Tanganyika
Serikali yaimarisha hatua za kudhibiti bei za Mafuta
Kamati kuu CCM yampitisha Mtafikolo kugombea ubunge Isimani