📌 asilimia 28.6 ya watanzania wana nishati safi ya kupikia.
Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Tanzania imeendelea kujinadi Kimataifa kwa kuwasilisha mafanikio yake katika Matumizi ya Nishati safi ya kupikia, ambapo hadi kufikia mwaka 2025, asilimia 28.6 ya Wananchi wana nishati safi ya kupikia, hatua inayoonesha ongezeko kubwa la matumizi hayo nchini.
Mafanikio hayo yameelezwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu (Wizara ya Nishati) , Mhandisi Innocent Luoga katika Mkutano wa 5 wa mwaka wa Kamati Maalum ya Wataalamu ya Umoja wa Afrika kuhusu Nishati na Uchukuzi unaoendelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini leo tarehe Aprili 28, 2026.
Kamishna Luoga amesema hatua hiyo imechangiwa na juhudi za makusudi za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, Serikali imezindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034 unaolenga kufikisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku utekelezaji wake ukijikita katika kampeni za uhamasishaji zinazolenga kuwafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji.
Aidha, Serikali inaendelea kutoa ruzuku katika mitungi na majiko banifu ili kupunguza gharama kwa wananchi, sambamba na kuhamasisha taasisi za umma na binafsi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi, mkaa mbadala, biogesi, na umeme.

Hatua hizo zimepokelewa vyema na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ambazo zimeipongeza Tanzania kwa jitihada zake katika kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwa kinara wa agenda hiyo, hatua inayochangia kulinda mazingira, afya za wananchi na kukuza maendeleo endelevu barani Afrika.


More Stories
Bodi ya REA yaridhishwa miradi mwambao ziwa nyasa
Shaka: Muungano ni sisi
Exim yafanya mazungumzo na wizara ya elimu kufadhili Wanafunzi elimu ya juu