April 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imewataka wafanyakazi kuwa Makini wawapo makazini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

ZAIDI ya wafanyakazi 169 wamefariki dunia wakiwa kazini kutokana na ajali na magonjwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia 2023 hadi 2025.


Mbali ya vifo hivyo pia jumla ya ajali zilizoripotiwa Katika kipindi hicho zilizosababishwa na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ni 3,557.

Akizungumza na waandishi wa habari April 23 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu amesema l takwimu hizo ni kubwa na inaathiri shughuli za uzalishaji na kudidimiza uchumi wa nchi.

“Zinahitajika hatua madhubuti za kushughulikia changamoto hiyo, serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi ya Taifa kupitia taasisi ya OSHA, serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria za Afya na Usalama mahali pa kazi,” amesema Waziri Sangu.

Ameendelea kusisitiza, “lengo ikiwa ni kuhakikisha kwamba maneno yote ya nchini yanakuwa na mifumo Bora ya kuzuia ajali, magonjwa na vifo na hivyo kuwa na uzalishaji wenye tija na wafanyakazi wenye afya njema”.

Amesema ‎ kuzingatia hilo serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuendesha kampeni maalumu ya uhamasishaji mafunzo ya Usalama na afya mahala pa kazi.

“Tunapoelekea kilele Cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi April 28 mwaka huu, tutashirikiana na wadau kuendesha kampeni maalumu ya uhamasishaji kupitia shughuli mbalimbali,’ amesema Waziri Sangu.

Amesema kampeni hiyo itaendeshwa wakati ikielekea maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani ambayo inalenga kuhamasisha wafanyakazi na waajiri kushirikiana kuboresha mazingira ya kazi ili kuzuia madhara yanayotokana na shughuli za kazi.

“Serikali itaendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kulinda nguvu kazi ya taifa kwa kuibeba ajenda ya usalama na afya mahala pa kazi, huku ikitangaza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika kitaifa mkoani Njombe,” amesema Waziri Sangu

‎Amesema maadhimisho hayo nchini yalianza rasmi mwaka 2004 na yamekuwa yakifanyika kila mwaka yakiratibiwa na serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), kwa kushirikiana na wadau wa utatu ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Mazingira bora ya kazi kisaikolojia ni njia ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kujenga taasisi imara,” ikiwa inalenga kuhimiza umuhimu wa afya ya akili mahala pa kazi.

‎Waziri ameeleza kuwa changamoto za afya ya akili zinazohusiana na kazi zimekuwa zikiongezeka duniani, hali inayochangia kupungua kwa tija na kuathiri ustawi wa wafanyakazi.

Amenukuu takwimu za Shirika la Kazi Duniani zinazoonesha kuwa mamilioni ya wafanyakazi wanakabiliwa na matatizo hayo, hivyo kuna haja ya kuyapa uzito sawa na changamoto za kimwili.