Na Penina Malunzo,Timesmajira
AFISA Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia ,Dkt. Gladness Kirei ametoa wito kwa Jamii ikiwemo mashirika mbalimbali nchini kuwasaidia wanafunzi walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito na kisha kurudi katika mfumo rasmi wa elimu kuwasaidia changamoto zao wanazozipitia ikiwemo unyanyapaa kutoka kwa baadhi ya watu.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuona wingi wa wanafunzi hao ambao walianza kurudi shule kama waraka wa elimu ulivyowataka mwaka 2021 kuanza kuacha shule kutokana na unyanyapaa (Stigma)wanazokumbana nazo kwa jamii,walimu pamoja na wanafunzi wenzao.

Akitoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kukabiliana na Changamoto ya Unyanyapa kwa wanafunzi wanaorudi shuleni kutokana na Changamoto mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito iliyozinduliwa na Taasisi ya Msichana Initiative.
Dkt.Kirei amesema wapo wanafunzi ambao wanashindwa kuendelea na masomo kwasababu ya unyanyapaa kutokana na kufanya wanafunzi hao kutojisikia vizuri.”Muongozo unaeleza wazi kuwa mwanafunzi anapoona shule moja inamuonyesha unyanyapaa au watu fulani wanafanya hivyo,ni ruhusa kuhama shule kwani muongozo unamruhusu.

”Tunaipongoza Shirika la Msichana Initiative kwa kuwapambania wasichana hadi kuona wale wanaokuwa na ujauzito wanarudi shuleni hivyo kupitia kampeni hii iliyozinduliwa leo inaenda kuhamasisha jamii kuona kundi hili kama wanafunzi wengine na kuwaacha wasome ili kufikia ndoto zao,”amesema
Aidha amesema kuna umuhimu wa kuwasaidia kwa njia mbalimbali ikiwemo kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali ,vifaa vya shule pamoja na kuwatia moyo ili waweze kufikia malengo yao.
Dkt. Kirei amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi hususan mtoto wa kike kupata elimu iliyobora bila kunyanyapaliwa ili waweze kutimiza ndoto zao.

Kwa Upande wake Mkurugenzi mpya wa Msichana Initiative,Consolata Chikoti amesema wao kama shirika wamekuwa wakifanya kazi za kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha wanaangalia changamoto wanazokabiliana nazo watoto wa kike na kuhakikisha wanazitatua na kuwalinda.
”Utekelezaji wa ‘Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021’ unaoruhusu kurejea shuleni kwa wanafunzi walioacha shule kutokana na sababu zozote zile ikiwamo mimba kurudi katika mfumo rasmi wa elimu,umekuwa na changamoto mbalimbali wanazopata katika jamii.
”Takwimu zilizofanywa na Wizara ya Elimu zinaonesha kwamba Watoto ambao walikuwa wameingia kwenye mfumo wa shule baada ya kudondoka walikuwa takribani watoto wa kike 58,huku takwimu za Global Women Institute zinaoesha kwamba takribani wasichana Milioni 60 wamekutana na ukatili wa kijinsia huku Tanzania takribani wasichana Milioni 14.6 wanakumbana na changamoto mbalimbali za kuwakwamisha kupata haki ya elimu,”amesema

Aidha amesema takwimu pia zinaonesha kwamba msichana mmoja kati ya watatu anaolewa kabla ya kutimiza miaka 18 huku msichana mmoja kati ya wanne anauwezo wa kumaliza shule ya sekondari,huku wapo wasichana wanaokosa shuleni siku nne hadi tano kutokana na changamoto zinazotokana na hedhi.
Chikoti amesema wao kama shirika wamekuwa wakiona vikwazo vingi vinavyomkuta msichana na wao wanajitahidi kuvitatua katika mradi wao wa rudi shule wamewafikia zaidi ya wasichana 500 na mwaka huu wanatarajia kuwafikia wanafunzi 250 ambapo wamegundua katika utekelezaji wa mradi huo kwani wasichana wanakumbana na changamoto ya unyanyapaa pale wanaporudi shuleni kutoka kwa wanafunzi wenzao,jamii na wakati mwingine kwa walimu

Mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika uzinduzi wa kampeni hiyo,Theresa Juma (21) amesema licha ya changamoto anazozipitia na kupata ujauzito akiwa na umri wa miaka 18 akiwa amemaliza kidato cha kwanza lakini ametamani kurudi shule na sasa anaendelea na masomo yake huku akiwa na mtoto wake.
”Nikikumbuka naumia sana niliacha shule nikiwa naingia kidato cha pili ambapo nilifaulu na kupata Daraja la Kwanza nilipopata ujauzito,nilifukuzwa nyumbani na niliangaika sana,nimeamua kujitafutia maisha huku nikijisomesha mwenyewe nikiwa nalipa ada na kuendesha maisha yangu,”amesema

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati