Na Mwandishi wetu,Timesmajira
IMEELEZWA kuwa mradi wa uwekezaji wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mzizima Towers unaotekelezwa jijini Dar es Salaam na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefikia asilimia 91 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Desemba 31 mwaka huu.
Taarifa hiyo imetolewa rasmi jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipowasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Sangu, imesema mradi huo wa uwekezaji unahusisha ujenzi wa minara miwili, ikiwemo mnara wa biashara wenye ghorofa 35 na mnara wa makazi wenye ghorofa 32, ukiwa na jumla ya eneo la ujenzi la mita za mraba 95,018.15.
Katika taarifa hiyo imesema majengo hayo yamebuniwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya usanifu wa kimataifa ili kukidhi mahitaji ya biashara, makazi na huduma za utalii katika jiji hili la Dar es Salaam.

Waziri huyo ameongeza kwa kusema kuwa mradi huo utakapokamilika utakuwa na hoteli ya hadhi ya nyota tano itakayoendeshwa na Radisson Hotel Group, yenye jumla ya vyumba 156 vya kulala pamoja na vyumba 132 vya makazi ya muda mfupi (hotel apartments).
Sangu amesema mradi huo unatekelezwa kwa asilimia 100 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kama sehemu ya mkakati wa Mfuko huo kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati yenye tija kwa wanachama na Taifa kwa ujumla.

Amebainisha kuwa uwekezaji huo unalenga pamoja na kuongeza thamani ya mali za Mfuko pamoja na kuimarisha uwezo wake wa kulipa mafao kwa wanachama.
Akizungumza baada ya ziara ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Hawa Mchafu Chakoma, amesema wajumbe wa kamati hiyo wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua mradi huo kuendelea kutekelezwa nchini ili uweze kuleta tija kwa Mfuko na Taifa kwa ujumla.
“Sisi kamati tumefika hapa na kujionea kazi inayofanyika katika mradi huu. Kazi ni nzuri sana na inaonyesha kuwa uongozi wa NSSF chini ya Mkurugenzi Mkuu, Bw. Masha Mshomba, umekuwa mfano wa kuigwa katika usimamizi wa miradi,” amesema. Hawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kufanya ziara ya kikazi na kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika mradi huo.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Kafiti Kafiti waliipongeza NSSF kwa uwekezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Naye Kangi Lugola amesema mradi wa Mzizima Towers ni uwekezaji muhimu wenye tija kubwa kwa Mfuko na Taifa kwa ujumla, akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kwa usimamizi mzuri wa Mfuko na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mradi wa Mzizima Towers unatarajiwa kuleta manufaa makubwa nchini kiuchumi ikiwemo kuongeza mapato ya Mfuko na Serikali, kuimarisha sekta ya biashara na utalii jijini Dar es Salaam pamoja na kuongeza ajira, ambapo zaidi ya wafanyakazi 300 wameajiriwa wakati wa ujenzi wa mradi huo, huku ajira zaidi ya 250 zikitarajiwa kupatikana mara baada ya kuanza kwa shughuli za hoteli na biashara ndani ya jengo hilo.

More Stories
Airtel Tanzania yaendelea kuimarisha Dhamira ya kukuza uchumi wa Kidijitali na Thamani kwa Wanahisa Katika Mkutano wa Minority Interest Forum 2026 Arusha
Watakiwa kuondoa dhana potofu kuhusu chanjo ya polio
Waandishi wahimizwa kuandika kwa maslahi ya taifa