Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema Serikali pia ipo katika hatua za mwisho za majadiliano ya utekelezaji wa Mradi wa uchakataji na usindikaji wa gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) unaotarajiwa kugharimu takribani dola za Marekani bilioni 42.
Mradi huo umetajwa kuwa ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati na unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara ya gesi katika ukanda na kimataifa.

Hayo yamebainishwa jijini hapa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mussa Makame wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi na fursa kwa vijana mwaka 2025/26 ambapo amesema
kuwa TPDC tayari imeanza maandalizi ya kitaasisi na kiufundi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuimarisha rasilimali watu, mifumo na usimamizi wa miundombinu.
Aidha amesema Shirika hilo pia linaendelea na mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vipya vya gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara unaolenga kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini.
Ambapo amesema kuwa uchorongaji wa kisima cha kwanza ulianza Februari 6, 2026 na hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 27 huku mradi huo ukitarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi kwa takribani futi za ujazo milioni 45 kwa siku.
“TPDC inaendelea kutekeleza mradi wa uchorongaji wa visima katika kitalu cha Ruvuma (Ntorya) pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Ntorya kwenda kiwanda cha kuchakata gesi Madimba mkoani Mtwara.
“Mradi huu utasaidia kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 60 na utaimarisha usalama wa nishati nchini,”amesema Makame.

Makame amesema kuwa Shirika pia linaendelea na mradi wa uchukuaji wa taarifa za mitetemo ya mfumo wa 3D katika kitalu cha Lindi-Mtwara kwa lengo la kubaini maeneo yenye uwezekano wa kuwa na mafuta au gesi asilia.
Amefafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 107 na utasaidia kuongeza uwezekano wa ugunduzi mpya wa rasilimali za gesi nchini.
Makame amesema kuwa upanuzi wa matumizi ya gesi asilia majumbani ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, ambapo hadi sasa nyumba zaidi ya 2,500 zimeunganishwa na mtandao wa mabomba ya gesi asilia.
Ameongeza kuwa miradi hiyo pia inaendelea kufungua fursa mbalimbali za ajira, mafunzo na ushiriki wa vijana katika sekta ya nishati huku akibainisha kuwa takribani asilimia 79 ya wafanyakazi wa TPDC ni vijana.
Aidha amebainisha kuwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, vijana wanapata fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, mafunzo ya vitendo pamoja na ushiriki katika zabuni za huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya mafuta na gesi nchini.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa mafuta nchi, Makame , amesema kuwa mafuta ya petroli na dizeli yanapatikana nchini kwa wingi na hakuna changamoto yoyote inayotarajiwa kuwaathiri wananchi, hata katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia mvutano wa vita katika eneo la Mashariki ya Kati.
“Kwa sasa changamoto ndogo inayoweza kujitokeza ni ongezeko la bei ya mafuta kutokana na mabadiliko ya soko la kimataifa, hata hivyo serikali kupitia Wizara ya Nishati tayari imeweka mipango ya dharura ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa wananchi,”amefafanua.

More Stories
Mahundi azindua kamati kuwasaidia wenye uhitaji
Mahundi,Child Support watoa msaada shule Jumuishi
Serikali yawekeza zaidi ya bil.32 Maabara ya Mkemia Mkuu