Na Penina Malundo,Timesmajira
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimeikumbusha jamii kuwa suala la ukatili wa kijinsia si jambo la kawaida wala la kiafya katika jamii kwani linavunja haki za binadamu na kudhoofisha ustawi wa watu, hususan wanawake na watoto.
Aidha, chama hicho kimewataka wazazi na walezi kuhakikisha hawawaweki watoto katika mazingira hatarishi yanayoweza kuhatarisha uhai wao au kuharibu afya zao ya akili na mwili.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Iftari ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani (IWD) iliyoandaliwa na TAMWA, ambayo iliwakutanisha waasisi na wanachama wa chama hicho kwa lengo la kuangazia safari ya miaka 39 ya TAMWA katika kutetea haki za wanawake na watoto wa kike nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema katika miaka ya hivi karibuni ukatili wa kijinsia umebadilika na kwa kiasi kikubwa umehamia katika mitandao ya kijamii, hali inayohitaji juhudi za pamoja kukabiliana nayo.
Amesema licha ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na TAMWA na wadau wengine katika kupinga ukatili wa kijinsia, bado changamoto hiyo inaendelea kujitokeza kwa sura mpya.

“Tunashukuru kuwa habari hizi zinawafikia wananchi na jamii ili waweze kubadilika. Mambo mengi yamefanyika kupitia TAMWA, lakini bado kuna mabadiliko ya tabia za ukatili ambapo zinaendelea kujitokeza kwa aina tofauti,”Amesema.
Amesema kuwa kwa sasa ukatili wa kijinsia umehama kwa kiasi kikubwa kutoka katika mazingira ya kawaida na kuhamia katika majukwaa ya mitandao ya kijamii, ambako kasi yake imekuwa kubwa.
Dkt. Reuben amesema waandishi wa habari wataendelea kutumia kalamu zao kupinga ukatili wa kijinsia katika mitandao, huku akiitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na taasisi nyingine zinazodhibiti mawasiliano kushirikiana kuweka mifumo na sheria madhubuti za kudhibiti maudhui yanayochochea ukatili wa kijinsia.

“Ni muhimu mamlaka hizi kukaa pamoja na kuweka sheria zitakazolazimisha makampuni makubwa yanayomiliki majukwaa ya mitandao kuhakikisha yanazuia matamko au ujumbe unaohamasisha ukatili wa kijinsia,” amesema.
Ameongeza kuwa iwapo hatua hizo zitachukuliwa na mifumo ya kudhibiti maudhui itawekwa kwa lugha mbalimbali na wakati wote, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ukatili wa kijinsia mtandaoni.
“Jumbe nyingi zinazoandikwa mitandaoni si tu kwamba zinawaumiza wale wanaolengwa moja kwa moja, bali pia zinaumiza wengine wanaozisoma,” amesisitiza.

Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Dkt. Reuben amesema TAMWA imepanga matukio mbalimbali ikiwemo kukutana na waasisi wa chama hicho pamoja na wanachama wachache ili kusimulia na kuhifadhi historia ya mwanzo wa TAMWA na mchango wa wanachama wake.
Amesema pia chama hicho kitapanga shughuli nyingine za kijamii ikiwemo kuwatembelea akina mama wafanyabiashara wadogo kama wamama wa mbogamboga pamoja na kufanya matendo ya huruma, hasa ikizingatiwa kuwa kipindi hiki ni cha Kwaresma na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Dkt. Reuben amesema anatamani kuona TAMWA inaendelea kukua na kufikia hata miaka 80 au 100 ijayo huku ikiendelea kusimama imara katika kutetea haki za wanawake, wasichana na watoto.
“Bado kuna mawanda mengi ambapo makundi haya yanahitaji kutetewa na kuendelezwa ili yaweze kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya uchumi,” amesema.

Kwa upande wake, mmoja wa waasisi wa TAMWA, Fatma Aloo, amesema chama hicho kilianzishwa rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo waandishi wa habari wanawake waliamua kuungana kupaza sauti dhidi ya dhuluma zilizokuwa zikiwakumba wanawake katika jamii.
“Sasa ni miaka 39 tangu kuanzishwa kwa TAMWA. Wakati huo tulikuwa vijana wadogo lakini tuliona wazi kuwa dhuluma nyingi zilikuwa zikifanywa dhidi ya wanawake, hata ndani ya familia. Hali hiyo ilituumiza na kutusukuma kuanzisha TAMWA kama jukwaa la waandishi wa habari kupigania haki hizo,” amesema.
Amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupambana na ukatili wa kijinsia, bado changamoto hiyo ipo na hivyo kizazi cha sasa na kijacho kinapaswa kuendelea kupinga ukatili huo, hususan unaochochewa na mfumo dume.
“Wanawake na wasichana bado wanaumia kutokana na ukatili wa kijinsia, hivyo mapambano haya yanapaswa kuendelea ili kuhakikisha haki zao zinalindwa,” amesema

More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro