
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
Mkoa wa Rukwa umepokea shilingi Bil. 20.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na utawala bora katika kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere ameeleza hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Machi 3, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Mkoa umeendelea kuimarika katika ukusanyaji wa mapato.
Taarifa iliyotolewa katika kikao hicho imeonesha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Mkoa wa Rukwa imekusanya shilingi Bil. 54.006, sawa na asilimia 117 ya lengo, huku Halmashauri za Mkoa zikikusanya zaidi ya shilingi bilioni 11.19, sawa na asilimia 70 ya lengo.
Wananchi wamehimizwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuchochea maendeleo endelevu ya Mkoa.
Katika sekta ya elimu, Mkoa umeendelea kufanya vizuri ambapo ufaulu wa Kidato cha Nne umefikia asilimia 96.3, huku shule za msingi zikionesha ongezeko la kiwango cha ufaulu, hali inayodhihirisha jitihada zinazoendelea za kuboresha huduma za kijamii.
Aidha, uongozi wa Mkoa umehimiza kuimarishwa kwa utunzaji wa mazingira na upandaji miti, pamoja na kuendelea na maandalizi ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 kinachotarajiwa kufanyika Mkoani Rukwa.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama