Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Shinyanga
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimeridhishwa na mradi wa Bandari kavu ya Isaka, iliyopo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, uliogharimu zaidi Sh. Bil 10.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi huo, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Kenani Kihongosi, amewataka wananchi hususani walio karibu na eneo la mradi huo, kulinda miundombinu hiyo, huku akibaimisha kuwa kuwa kutokuilinda ni sawa na kuihujumu Isaka na nchi nzima kwa ujumla.
“Kama kutakuwa na uhalifu utakaofanyika katika mradi huu maana yake mtakuwa mnarudisha nyuma maendeleo yenu, hivyo wajibu wenu ni kushirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na Serikali kwa ujumla kulinda bandari hii kwa manufaa yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo” amesema Kihongosi.
Pia amezitaja baadhi ya faida za mradi huo kuwa ni pamoja kusaidia urahisishaji wa usafirishaji wa mizigo kwa nchi jirani ikiwemo Uganda, Rwanda na Burundi, akieleza kuwa shughuli hizo zitafanyika katika bandari hiyo tofauti na awali ambapo ililazimu shughuli hizo kufanyika katika bandari ya Dar es Salaam.
Pia, ametoa wito kwa uongozi wa bandari na Mbunge wa Jimbo la Msalala, Johnson Magangila, kuhakikisha mradi huo unatoa kipaumbele kwa wazawa wa maeneo hayo, ambao ni wakazi wa Isaka na Kahama.
“Nitoe wito kwenu kuhakikisha mradi huu wa bandari vipaumbele vinatolewa kwa wazawa wa maeneo haya yani vijana na Isaka na Kahama kwani wageni wakiwa wengi na wenyeji wakiwa wachache italeta mgogoro kwa sababu watu wataona wananyang’anywa haki zao za msingi kwenye ardhi yao”, amesema Kihongosi.
Sambamba na hayo, Kihongosi ameendelea Kusisitiza kwa wananchi juu ya kulinda amani ya nchi, huku akiwataka vijana kutokubali kutumika kuwa sehemu ya uvunjifu wa amani ya nchi.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama