March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NBAA yatoa Elimu kwa Wanafunzi ili kuongeza tija katika taaluma ya uhasibu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuwajengea ufahamu kuhusu kazi za Bodi na kukuza taaluma ya uhasibu nchini.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA, CPA Kulwa Malendeja, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, CPA Pius Maneno, amempongeza chuo kilichoshirikiana na Bodi hiyo kwa kuwaleta wanachuo wanaosoma masomo ya uhasibu na biashara ili kupata elimu ya vitendo kuhusu kazi za Bodi.

Malendeja amesema kuwa ili kuwa Mhasibu au Mkaguzi aliyeidhinishwa kisheria, ni lazima mtu apitie mitihani ya NBAA na kupata cheti cha kitaaluma, ambacho kinatambulika kitaifa na kimataifa, na kumwezesha kufanya kazi ndani na nje ya nchi.

“Nimefurahishwa kuona wanafunzi wa Sheria pia wakishiriki katika ziara hii, kwani wana nafasi ya kusomea masomo ya uhasibu na kuwa CPA (Certified Public Accountant),” alisema Malendeja.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya, amesema ziara kama hizi ni fursa kubwa kwa wanafunzi kupata taarifa mbalimbali kuhusu Bodi na huduma zake.

Pia aliongeza kuwa kupitia maoni ya wadau, NBAA imeamua kuanzisha mahafali mawili kwa mwaka badala ya moja tu, ili kupunguza ucheleweshwaji wa vyeti vya kitaaluma.

Dkt. Ayubu Timba, Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro, ameishukuru NBAA kwa mwaliko kwa wanafunzi na kueleza kuwa elimu iliyotolewa itawaongoza wanachuo na kuwapa dira sahihi katika taaluma ya uhasibu. Pia aliwasisitiza kuwa wanachuo hao wawe mabalozi wa taaluma yao kwa wenzao na jamii kwa ujumla.