March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yafikia asilimia 90 ya usambazaji umeme Vitongoji Kilimanjaro

Serikali yafikia asilimia 90 ya usambazaji umeme

Na Joyce Kasiki,Dodoma

SERIKALI  imesema imepiga hatua kubwa katika kusambaza umeme katika vitongoji vya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo hadi kufikia Januari 2026 jumla ya vitongoji 2,032 kati ya 2,258, sawa na asilimia 90, tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.

Hayo yameelezwa bungeni na Naibu Waziri wa Nishati Salome Mkamba  wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,  Esther Edwin Malleko, aliyeuliza mkakati wa Serikali wa kumaliza usambazaji wa umeme katika vitongoji vyote vilivyosalia mkoani humo.

Akijibu swali hilo, Makamba amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya umeme kwa lengo la kufikisha huduma hiyo katika vitongoji vyote vilivyosalia.

Amefafanua kuwa vitongoji 226 ambavyo bado havijapatiwa umeme vitafikiwa kupitia miradi miwili tofauti. Kati ya hivyo, vitongoji 40 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili A  huku vitongoji 186 vikitarajiwa kufikiwa kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B

Waziri huyo amesisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha kufikisha umeme katika vitongoji vyote 2,258 vya Mkoa wa Kilimanjaro, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa mkoa huo.

Makamba  kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wote, hususan maeneo ya vijijini, kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya maendeleo jumuishi na uchumi wa viwanda.