April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mulamula amuaga Balozi wa Canada baada ya kumaliza muda wa uwakilishi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), ameagana na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Balozi O’Donnell Waziri Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji kazi wake ambao umewezesha Serikali ya Tanzania na Canada kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu pamoja na biashara na uwekezaji.

Waziri Mulamula ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Canada ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa na Balozi O’Donnell wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi hapa nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell amesema anajivunia uwepo wake Tanzania, amejifunza mengi ikiwemo ukarimu wa Watanzania na amewashukuru Watanzania kwa upendo mkubwa waliomuonesha katika kipindi chote cha uwakilishi wake nchini.

Pamoja na mambo mengine, Balozi O’Donnell ameihakikishia Tanzania kuwa Canada itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya gesi pamoja na biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kadhalika, Balozi O’Donell amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania ya kuimarisha ukuaji wa Uchumi, utoaji wa huduma bora za afya, elimu ya msingi bure kwa watanzania pamoja na kuboresha miundimbinu kwa maendeleo ya watanzania.