April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa mafuta ya kula wapatao 972 wapatiwa elimu Nyanda za Juu Kusini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

WAZALISHAJI wa mafuta ya kula wametakiwa kufuata kanuni bora za
kilimo, usindikaji na zile za afya ili kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa hiyo nchini.

Wito huo ulitolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati wa
mafunzo kwa wasindikaji, wauzaji, wasambazaji na wenye maduka yanayouza mafuta wapatao 972 yaliyofanyika katika mikoa minne ya Nyanda za Juu Kusini kuanzia Februali 19 hadi 29, mwaka huu.

Mafunzo hayo yalihusisha wadau hao kutoka Mikoa ya Iringa, Njombe,
Songwe na Mbeya ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kupitia
Wizara ya Viwanda na Biashara kutaka wazalishaji wa mafuta nchini
kusaidiwa ili waweze kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Kwa sasa mafuta ya kula yanayozalishwa nchini ni tani 200,000 kwa
mwaka, wakati mahitaji halisi ni tani kati ya 400,000 hadi 600,000.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na BRELA, SIDO na Wakala wa Vipimo (WMA), ambapo kila mmoja alieleza wadau hao nafasi yake katika kufanikisha uzalishaji na ukuzaji biashara ya mafuta.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa TBS, Baraka Mbajije, amewataka wazalishaji wa mafuta kufuata kanuni bora za kilimo, usindikaji pamoja na za afya.

Zao la alizeti

Mbajije amesema kanuni bora za kilimo zinahusisha mbegu bora, kuvuna kwa wakati na mazao yanayovunwa kwa ajili ya uzalishaji mafuta yanatakiwa yawe yamekomaa.

Kwa upande wa kanuni bora za usindikaji kwa mujibu wa Mbajije ni
pamoja na kuzingatia usafi hasa kwenye mazingira ya viwandani. Amesema mazingira ya uzalishaji viwandani yanatakiwa kuwa safi pamoja na mashine zinazotumika.

Akizungumzia kanuni bora za afya, Mbajije amesema wazalishaji
wanatakiwa kuhakikisha vifaa vya kuhifadhi mafuta ni safi ikiwa ni
pamoja madumu yanayotumika kihifadhi mafuta hayo yawe yamesafishwa
vizuri.

“Madumu wanayoweka mafuta wahakikishe wameyafisha vizuri na waweke
rebo zinazoeleza bidhaa hizo ni za aina gani,” alisema na kuongeza
kwamba haikubaliki kwenye madumu ambayo wazalishaji wanaweka mafuta iwe na rebo inayohusu bidhaa nyingine.

Aidha, amesema mafuta ya kula hayatakiwi kuwekwa juani, kwani
yanapokuwa juani kuna kemikali zinazozalishwa na zinaweza kusababisha magonjwa, ikiwemo kansa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Abel
Mwakasonda, alitoa mwito kwa kwa wadau hao kusajili TBS majengo ya
bidhaa za vyakula na vipodozi.

Amesema kwa kufanya hivyo, shirika hilo litaweza kuwafikia kwa
urahisi. “Tunatoa mwito kwa wadau kufika TBS, wasiogope kama kuna
makosa tutawasaidia kuyarekebisha,” alisema Mwakasonda.

Amesema ni muhimu kwa wafanyabiasha kusajili bidhaa na majengo ya
vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na
mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019.

Sheria hiyo ilirudisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA).

Amesema usajili wa bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria ili kuwawezesha kufanyabiashara zao urahisi.

Usajili majengo ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza bidhaa na wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazoenda kuhifadhiwa humo.

Kwa upande wa usajili wa bidhaa, eneo linalohusika ni bidhaa za
chakula na vipodozi. Usajili wa vipodozi unalenga kuhakikisha vipodozi vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania haviingizwi nchini kutokana na kuwa na viambata sumu.

Mafunzo hayo kwa wazalishaji wa mafuta ni mwendelezo wa mafunzo
yaliyokwisha kutolewa katika mikoa Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma.