April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAWA wajenga vyumba vya madarasa, ofisi ya walimu Usinge

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAMLAKA ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga vyumba 2 vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Usinge wilayani Kaliua Mkoani Tabora ili kuboresha sekta ya elimu.

Akikabidhi madarasa na ofisi hiyo hivi karibuni kwa niaba ya Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi, Kamanda wa Pori la Akiba la Moyowosi Daud Mnyampwani alisema mradi huo umegharimu jumla ya sh mil 50.

Alibainisha kuwa wamejenga madarasa hayo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha watoto wote walioandikishwa kuanza darasa la kwanza wanapata nafasi katika shule hiyo.

Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifadhili miradi ya maendeleo katika Mikoa na Wilaya mbalimbali ili kuwezesha jamii kupata huduma stahiki katika maeneo yao.

‘Tutaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya jamii, tunaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kuacha kuvamia mapori ya hifadhi za serikali ili kulinda uoto wa asili’, alisema.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Michael Nyahinga aliishukuru Mamlaka hiyo kwa kuwa mdau mzuri wa maendeleo ya wananchi katika wilaya hiyo na kuomba wadau wengine kuiga mfano huo.

Aliwataka walimu na wanafunzi wa shule hiyo kutumia vizuri vyumba hivyo ili viwe chachu ya kuongeza ufaulu wao na kuwawezesha kutimiza malengo yao ya kitaaluma.

Aidha aliiomba TAWA kuendelea kusaidia jamii kwa kutekeleza miradi mbalimbali ili kupunguza kero za wananchi katika sekta za afya, maji na nyinginezo.

Pichani ni moja ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Magharibi katika shule ya msingi Usinge Wilayani Kaliua Mkoani Tabora. Picha na Allan Vicent.