April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kushirikiana na CCBRT kuboresha Diplomasia ya Afya

Na Waandishi wetu, TimesMajira Online,Dar
Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeahidi kushirikiana na Hospitali ya CCBRT kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya nchini kupitia utekelezaji wa Diplomasia ya Afya.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali hiyo kwa lengo la kujionea shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa hospitalini hapo leo Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mulamula ameupongeza Uongozi wa Hospitali hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia watanzania hasa kuwapa akina mama tumaini la maisha hususan wanaopatwa na changamoto ya ugonjwa wa fistula.

“Wizara ninayoisimamia ni mtambuka na mchango wake umekuwa mkubwa ambapo nyinyi ni wadau wetu, tutashirikiana na Balozi zetu nje kuona ni jinsi gani tutapata wadau/washirika wa maendeleo watakaosaidia katika kuboresha sekta ya afya hususan hapa CCBRT,” amesema Waziri Mulamula.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBT, Brenda Msangi amesema kuwa pamoja na jitihada ambazo Serikali imekuwa ikizichukua kuboresha sekta ya afya nchini, hospitali hiyo pia inajitahidi kuboresha huduma zake na mazingira yake kwa ujumla ili kuweza kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi.

“Tunajitahidi kuwahudumia watanzania kadri tuwezavyo ila tunakabiliwa na baadhi ya changamoto za msaada wa utoaji wa huduma, vifaa tiba pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wetu ili kuweza kuboresha huduma zaidi,” amesema Bibi. Msangi.

Julai 05, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la kutolea huduma ya afya ya mama na mtoto katika hospitali ya CCBRT alisema kuwa katika mikakati ya kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga, Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma vya madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi wameanzisha mfumo wa kupitia takwimu za vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua lengo likiwa ni kuboresha zaidi huduma katika sekta ya afya.